Na Mwantanga Ame
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar leo itaanza kuwalipa wananchi 2,470 fedha zilizotokana na michango ya kuwasaidia walioathirika na ajali ya meli ya Mv. Spice Islander I.
Hatua hiyo serikali inaichukua baada ya kukamilisha zoezi la kufanya uhakiki majina ya watu waliojitokeza kudai kuwamo katika ajali hiyo.
Hapo awali ripoti ya Tume ilibaini kuwa meli hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Nahodha wake Said Abdallah Kinyanyite, ilipakia abiria 2470 na tani za mizigo zisizojulikana ambapo watu 203 walifariki na maiti zao kupatikana, maiti 159 zilitambuliwa na 44 hazikutambuliwa, na watu 941 na waliokolewa hai na watu 1370 wameripotiwa kupotea.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed, akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alisema fedha hizo rasmi zitaanza kutolewa leo, baada ya kukamilisha zoezi la uhakiki wa wanaostahiki.
Alisema serikali imeamua kuanza kutoa malipo hayo kwa wananchi baada ya kukamilisha kazi hiyo ambapo mgao wa kwanza utafanyika kwa majaribio katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema wananchi katika zoezi hilo watalazimika kuwa na vitambulisho vya Mzanzibari huku watoto wakiwa na wazee wa familia zao.
Alisema serikali haitamvumilia mwananchi yoyote atakayejaribu kufanya udanganyifu katika zoezi hilo kwa vile tayari imeshachukua hadhari mbali mbali kufanikisha zoezi hilo.
Alisema utoaji fedha hizo utafanyika katika vituo maalum ambavyo vimewekwa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo ambapo wananchi wataweza kutambuliwa na masheha wao.
Alisema fedha ambazo zinatarajiwa kutumika ni shilingi Bilioni 1.270 ikiwa zimetokana na michango ya wananchi mbali mbali, ikiwemo misaada ya taasisi za kibenki, Mashirika ya ndege, Vyama vya Siasa, watu binafsi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Zoezi hilo Waziri Aboud, alisema litaendeshwa hatua kwa hatua katika Mikoa mingine ili kuweza kuhakikisha kila muhusika anafikiwa bila ya matatizo.
Tayari serikali imeshachukua hatua mbali mbali za kulishughulikia suala hilo, baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi ya Tume ilioundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Baadhi ya hatua ambazo serikali imeshazichuka ni pamoja na kuiachia sheria kuchukua mkondo wake, ambapo tayari wahusika kadhaa wamepandishwa Mahakamani waliotajwa kuhusika katika tukio hilo wakiwemo wamiliki wa meli hiyo, watendaji katika Bandari ya Zanzibar, na Mawakala wengine ambao kwa siku ajali hiyo ikitiokea wakiwa kazini.
Mbali ya hatua hiyo pia serikali imefanya mabadiliko kwa baadhi ya watendaji wakuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, pamoja na kuwachukulia hatua za kinidhamu wafanyakazi waliotajwa katika ripoti hiyo.
No comments:
Post a Comment