Habari za Punde

Wanahabari Wasaidie Upatikanaji Haki, Utawala Bora

Na Salum Vuai, Maelezo

VYOMBO vya habari vimeelezewa kuwa na nafasi kubwa katika kuhamasisha utekelezaji wa maazimio ya haki za binadamu na utawala bora nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (CHRAGG), Jaji Mkuu Mstaafu Amiri Manento katika warsha ya siku moja ya kutathmini ripoti ya Tanzania kuhusu haki za binadamu iliyowasilishwa Geneva mwaka uliopita.

Katika warsha hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ya kimataifa jijini Dar es Salaam (DICC), Manento alisema waandishi wa habari wana jukumu kubwa na muhimu katika kuimarisha suala la uwazi na uwajibikaji ili kuisukuma serikali na watendaji wake wakuu kuwa makini katika kuwapatia raia haki wanazostahili.

Jaji huyo alifahamisha kuwa, endapo vyombo vya habari vitawajibika ipasavyo na kufanya kazi bila woga, matatizo mengi yanayokwaza upatikanaji wa haki na kuviza utawala bora nchini yataibuliwa na hivyo kupatiwa ufumbuzi.

"Waandishi wa habari ni lazima wajikite katika kuangalia utendaji na uwajibikaji wa watu waliopewa dhamana kubwa, aidha kufichua maovu ikiwemo rushwa, ufisadi na udhalilishaji, lakini kwa uwazi na kufanya uchunguzi wa kina na wa pande mbili", alisisitiza.

Aidha, alisema waandishi wana haki ya kuachiwa kufanya kazi zao katika mazingira yasiyokuwa ya hofu ya kuogopa kushitakiwa, kwa kupewa uhuru kamili wa kuogelea katika kutekeleza majukumu yao yenye manufaa kwa kila mwananchi.

Mapema, Katibu Mtendaji wa tume hiyo Mary Massay, alisifu hatua iliyofikiwa nchini Tanzania katika masuala ya haki za binadamu na utawala bora, hasa baada ya vigezo vingi vya kuimarisha hali hiyo nchini kukubaliwa na kupitishwa katika mkutano wa Geneva.

Miongoni mwa mambo ambayo Tanzania imeonekana kufanya vizuri ni pamoja na usimamiaji wa haki za watoto na watu walio katika makundi maalumu wakiwemo walemavu, uhuru wa kuabudu na nyenginezo.

Akizungumza baada ya mkutano huo, mtoa mada kutoka taasisi ya ARTICLE 19 Eastern Africa, Henry Maina, alisema wakati umefika jamii za Kiafrika zikumbuke wajibu wa kulindiana heshima, ili kuepuka migogoro ya kijamii iliyoanza kujitokeza na kutia hofu.

Maina alikuwa akizungumzia hali katika nchi yake Kenya, ambako kwa siku za hivi karibuni kumeibuka hofu kwa wanaume kukataa kuwasaidia wanawake au kusaidiwa wao katika usafiri wa magari kwa shaka ya kutekwa nyara na kufanyiwa vitendo viovu.

Warsha hiyo ilifanyika chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Canada nchini Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.