Na Khamisuu Abdallah
MRAJIS wa Vizazi na Vifo, Shaaban Ramadhan Abdalla amethibitisha kuwepo tatizo la watu wengi kuwa na vyeti feki vya kuzaliwa wakati wanapokwenda kuomba hati za kusafiria Idara ya Uhamiaji.
Mrajis huyo alithibitisha kuwepo kwa tatizo hilo baada ya Idara ya Uhamiaji hivi karibuni kubaini kuwepo kwa vyeti feki kwa baadhi ya wananchi wanaoomba hati za kusafiria.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mrajis huyo alisema Idara ya Uhamiaji huwalazimisha waomba hati za kusafiria vyeti vya kuzaliwa na wanapovipeleka ni feki.
“Idara ya Uhamiaji huleta vyeti vya kuzaliwa vya wanaoomba hati za kusafiria katika Idara yetu kwa ajili ya kuvichunguza kama ni halali, tumewahi kubaini kuwa vipo vyengine vimefojiwa”,alisema Mrajis huyo.
Alifahamisha kuwa watu wengi wamekuwa wakifoji vyeti vya kuzaliwa kwani ni rahisi kupatikana kuliko kusubiri utaratibu wa Idara ya Urajis, ambapo pia hawezi kufanikiwa kwani vyeti vya kufoji hubainika.
Mrajis huyo alisema wapo watu wamekuwa wakijishughulisha na utengenezaji wa vyeti feki vya kuzaliwa na kuwataka wananchi wawaepuke watu wa aina hiyo.
Naye Naibu Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar, Neema Mashaka katika siku za hivi karibuni limekuwepo tatizo la wananchi wengi wanaoomba hati za kusafiria kushindwa kuzipata baada ya kubainika kutumia vyeti za kuzaliwa visivyo halali.
Naibu huyo alisema kabla ya mwananchi anayeomba hati ya kusafiria kupewa sharti la muhimu ni kupata cheti cha kuzaliwa na anapokipeleka katika Idara hiyo, huchukuliwa hadi Idara ya Vizazi na Vifo kwa ajili ya kuangaliwa uhalali wake.
Alifahamisha kuwa wale wanaobainika kutumia vyeti feki vya kuzaliwa hunyimwa hati hizo na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Naibu huyo aliwataka wananchi kutojihusisha na udanganyifu wa kufoji vyeti vya kuzaliwa, ili kuepuka kuwasababishia kukosa haki zao za msingi.
No comments:
Post a Comment