Na Mwantanga Ame
NAIBU waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zahra Ali Hamad, ameshindwa kuzizuia hisia zake ndani ya kikao cha Baraza la Wawakilishi na kuangua kilio alipokuwa akielezea jinsi alivyoweza kufanya kazi vyema na waziri wake Ramadhan Abdalla Shaaban.
Kabla ya kufanya majumuisho ya mswada wa kuanzishwa Baraza la kutathmini elimu ya Zanzibar, Zahra alisema bosi wake huyo amekuwa mlezi mzuri katika utumishi tangu wafanye kazi pamoja katika wizara hiyo.
Naibu huyo alishindwa kuzuia hisia zake ambapo kila alivyojaribu kuelezea mahusiano yake ya kikazi na waziri huyo sauti yake ilibadilika na kuishia kufuta machozi.
Hatua hiyo imefikia baada ya hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kumteua Ramadhan Abdalla Shaaban kuwa waziri wa Ardhi Makaazi, Maji na Nishati.
Zahra alisema ameupokea uteuzi huo kwa hisia kubwa kutokana na kiongozi huyo kuwa ni mmoja ya waliomuonesha njia katika utumishi wake kwani aliingia katika wizara hiyo akiwa ni kipofu anayeona.
Alisema mengi ya mambo aliyokuwa akiyaamua kwa kuyafanyia kazi yalitokana na mchango wa waziri huyo jambo ambalo litamfanya kutomsahau akiwa anamuacha ndani ya wizara hiyo.
Alielezea matamshi hayo yakitoka kwa hisia kali huku akibugujikwa na machozi, ambapo baadaye alirudi katika hali ya kawaida na kuanza kujibu na kutoa ufafanuzi wa hoja mbali mbali za wajumbe wa Baraza hilo.
Nae Waziri wa wizara hiyo Ramadhan Abdalla Shaaban akijibu masuala ya wajumbe hao alielezea hisia zake kwa kumshukuru Naibu huyo kwa mchango aliompa katika utumishi wa wizara hiyo.
Alisema kwa kiasi kikubwa Naibu Waziri huyo hakuwahi kulumbana nae alipojaribu kumuelekeza baadhi ya mambo ya kazi na kikubwa alikuwa msikivu na mwenye kujenga heshima mbele yake.
Hata hivyo, alisema anatarajia Naibu huyo bado atapata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wajao wa wizara hiyo, ambapo sasa atafanya kazi na Ali Juma Shamuhuna ambae ndie aliyeteuliwa kushika nafasi ya Uwaziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali.
Naibu waziri huyo akijibu hoja za wajumbe hao alisema Wizara yake imekuwa ikipingana sana na walimu wanaoendesha skuli za masomo ya ziada ‘tuition’ kutokana na nyingi zake kuonekana kukiuka taratibu.
Alisema hivi sasa katika kuchukua hatua hiyo wameamua kuifunga skuli ya Darajani inayotoa masomo ya ziada baada ya kushindwa kutimiza masharti iliyowekwa na wizara hiyo juu ya muda.
No comments:
Post a Comment