Na Mwantanga Ame
ALIYEKUWA waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ramadhan Abdalla Shaaban, amezianika hadharani skuli zilizofutiwa matokeo ya kidato cha nne baada ya kudaiwa kufanya udanganyifu.
Waziri Shaaban, aliyasema hayo jana wakati akitoa ufafanuzi kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia mswada wa kuanzishwa kwa Baraza la Vipimo na kutathmini elimu ya lazima na mambo yanayohusiana na hayo.
Hatua ya Waziri huyo imekuja baada ya Wajumbe hao kutaka kujua ni watahiniwa wangapi waliofutiwa matokeo yao kati ya 3,303 kwa Tanzania nzima.
Waziri Shaaban alisema, katika uchunguzi uliofanywa imeonekana kuwapo kwa skuli nyingi zilihusika katika udanganyifu huo.
Akiweka hadharani suala hilo alisema kwa upande wa Unguja skuli zilizofutiwa matokeo ni pamoja na Chuo cha Kiislamu Mazizini, Chuo cha Kiislamu Pemba, Skuli ya Sekondari ya Jang’ombe, Hamamni, Pwani Mchangani na Bilal Muslim.
Skuli nyengine ambazo alizitaja ni pamoja na SUFA, Philter Federal, Regeza Mwendo, Fuoni, High View na Laurent.
Alisema kati ya waliofutiwa mitihani hiyo wawili walikuwa ni wa mtihani wa maarifa na watihaniwa 3,301 wa mtihani wa kidato cha nne ambvapo kwa upande wa Zanzibar ni 1,010 katika skuli 30 za serikali na binafsi.
Waziri huyo alisema kwa watahiniwa wa kujitegemea ni 1,056 na jumla ya waliofutiwa wote kwa Zanzibar ni 2076 ikiwa ni sawa na asilimia 62.9 na kwa Tanzania bara ni watahiniwa katika vituo 53 walifutiwa.
Kutokana na hali hiyo Waziri huyo aliishauri jamii kuacha vitendo vya udanganyifu katika mitihani kwani vimekuwa vikiichafulia sekta ya elimu Zanzibar na kuiondolea sifa ya kuwa na wataalamu wazuri.
Alisema hivi sasa baadhi ya mataifa imekuwa ikiwakataa wataalamu wa Kenya kutokana na kudaiwa kuwapo kwa wanafunzi wanaopata vyeti wakiwa hawana uwezo jambo ambalo haliwezekani na Zanzibar kuachiwa linde hivyo.
Waziri huyo alisema serikali katika kulifanyia kazi hilo hivi sasa inasubiri ripoti ya wataalamu waliopewa kufanya uchunguzi juu ya suala hilo na itahakikisha wataotajwa serikali itawachukulia hatua za kisheria.
Akiendelea Waziri huyo alisema adhabu iliyochukuliwa Wizara hiyo inapingana nayo na tayari walishaliomba baraza la Mitihani Tanzania kuliangalia suala hilo ambapo jana Waziri huyo alikuwa na mazungumzo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Tanzania Bara Dk. Shukuru Kawambwa.
Hata hivyo waziri huyo alisema suala la kulazimisha kuwa na Baraza la Mitihani la Taifa la Zanzibar bado haijawa dawa kwani vitendo vya udanganyifu vinaendelea kutokea na ni vyema wazazi kuacha mtindo wa kuwanunulia mitihani watoto wao na kuwa wepesi kutoa taarifa za madalali wa mitihani.
Akizungumzia mswada huo alisema Wizara hiyo hivi sasa inajiandaa kuona wanafunzi wanaopasi katika kidato cha pili kuwapo kwa uwazi wa matokeo yao pamoja na kuwa na mahafali ambayo watapewa vyeti vitavyokuwa vinatolewa na Bodi.
Wajumbe wa Baraza hilo waliupitisha mswada huo baada ya kufanya marekebisho mbali mbali ya tafsiri ndani ya sheria hiyo.
No comments:
Post a Comment