Na Husna Mohammed
WAANDISHI wa habari wametakiwa kuisaidia serikali katika kuibua matatizo mbalimbali yalioko katika jamii hasa vijijini.
Akizungumza na Zanzibar Leo, huko ofisi za TAMWA Mombasa nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Mkurugenzi wa Chama cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Ananilea Nkya, alisema waandishi wa habari ndio mdomo wa jamii katika kuwasemea wananchi hasa wa vijijini ambapo hawapati fursa ya kutoa maoni yao.
Alisema watu wengi wa vijijini hasa wanawake wamekuwa wakikosa mwamko mbalimbali katika suala zima la kudai haki zao katika jamii na hata taifa kutokana na uelewa mdogo walionao.
Mkurugenzi huyo, alisema pamoja na mambo mengine TAMWA, inataka kuona kwamba kunatokea mabadiliko kutokana na matatizo mbalimbali yanayowakumba wanawake.
“Mabadiliko yanaweza kutokea iwapo yatafichuliwa mambo yote yanayowadhalilisha wanawake na mtoto wa kike katika jamii hususan kwa kukosa fursa muhimu za kijamii kama elimu na hata kutoa mawazo katika jamii”, alisema.
Nkya alisema TAMWA, imekuwa mstari wa mbele kupambana na matatizo ya ubakaji, kulazimishwa wanafunzi kuolewa, wanawake kutoshirikishwa katika maamuzi, kutelekezwa kwa wanawake na watoto, vipigo kwa wanawake, ukeketaji na mambo mengine ya unyanyasaji wa kijinsia.
Alifahamisha kuwa kupitia TAMWA kwa kiasi kikubwa imeweza kuwakomboa wananchi wengi hasa wa vijijini wanaofanyiwa vitendo vya udahalilishaji katika maeneo yao wanayoishi.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alisema vyombo vya habari Zanzibar vimekuwa vikitoa mashirikiano ya kutosha katika suala zima la kupambana na unyanyasaji wa kijinsia.
No comments:
Post a Comment