Hivi karibuni Rais wa Zanzibar Dk
Ali Mohammed Shein alinukuliwa akitoa karipio kali kwa Mawaziri na watendaji
wasiotekeleza majukumu yao kwamba ima waondoke wenyewe kabla ya kuondoshwa na
Rais.
Dk Shein aliwataka watendaji wote
kutekeleza wajibu wao na kufanya kazi kwa bidii ili kuwaletea maendeleo wananchi
wa Zanzibar.
Kauli nzito kama hii kutoka kwa
kiongozi mkuu wa nchi inaashiria mambo mengi kwa wachambuzi wa habari.
Kwanza kuna viongozi wazembe
ndani ya Serikali wasiotekeleza wajibu wao ilhali walipoteuliwa kushika
nyadhifa hizi walitarajiwa na Rais kuwajibika ipasavyo.
Pili Kuna viongozi mzigo katika
Serikali wamebebwa, wamepewa dhamana, wamepewa semina elekezi na bado hawajijui
au hawajitambui kitu gani wanatakiwa kukifanya katika kukabiliana na majukumu
ya kazi zao.
Na tatu Mheshimiwa Rais anatumia
fursa ya mwisho kuwaonya mbele ya wananchi badala ya kuwaonya nyuma ya pazia
ili wajijue kwamba Rais anawafahamu na kuwafuatilia nyendo zao.
Inawezekana Rais alipopendekezewa
majina ya viongozi na watendaji aliowateua kushika nyadhifa tofauti alijenga imani kubwa kwao kama watakabiliana
na majukumu yao na kutekeleza wajibu wao kama watendaji kiufanisi si kwa malengo waliyowekewa tu bali kupita zaidi na hapo kuweza kuonekana
utendaji wao kinadharia na kivitendo. Hili linaonekana sasa kumtesa Rais na ni
yeye mwenye dhamana ya kuwaweka na kuwaondoa kwani aliyotarajia siyo
yanayotokea..
Dhana ya uwajibikaji Serikalini
ima haitambuliki au haitakiwi. Sote tulishuhudia maafa ya MV Spice hakuna
aliyewajibika mpaka ilipoundwa Tume.
Hivi karibuni Tume ya Baraza la Wawailishi
ilitoa hadharani taarifa ya uchunguzi ulioagizwa kufanywa na Baraza la
Wawakilishi ambayo iliwanyooshea vidole watendaji Serikalini wakiwemo Mawaziri
na Watendaji wangine wakuu. Serikali imeipokea na kuthibitishia itaifanyia kazi
na hili pia linaashiria nia njema ya Serikali kuvipa nafasi mihimili mengine ya
utawala kama Bunge na Mahakama kufanya kazi zake bila ya kuingiliwa na Serikali
kuu. Tusubiri tuone khatma yake.
Cheo ni dhamana si utajiri wala
ulwa. Cheo ni masuuliyah hatutoulizwa na waliotukabidhi tu dhamana bali pia
Muumba naye atakuja kutuuliza.
Hivi kweli kama ni wewe kiongozi/mtendaji
unaezembea au usiejibidiisha katika
kutekeleza dhamana na majukumu umemsikia aliyekuteuwa? Ulipoapa mbele ya Mheshimiwa Rais
ulielewa uzito wa kiapo chako? Ulipobeba Msahafu au Biblia ulifahamu maana na uzito wa kitabu kitakatifu wakati unaapa? Unapoingia Ofisini unajitathmini utendaji wako?
Mheshimiwa Rais, wananchi
tumekusikia tupo pamoja na wewe lakini kama rungu unalo mwenyewe tumekupa ridhaa kulitumia kwa maslahi
ya nchi na wananchi wa Zanzibar.
Kwetu Z'bar suala la kuwajibishana ni gumu kwani viongozi na watendaji wengi wa serikali wamechaguliwa ama kisiasa(watoto wa wanamapinduzi, au wazee wao walimuwezesha mzee kuingia madarakani) au anatoka shamba fulani.
ReplyDeleteKwa hivyo, Rais amesema lkn. utekelezaji ni 'issue'