Habari za Punde

Tausi Waondoka


Na Abdi Shamnah

WASANII wa kikundi cha Taarabu cha Tausi, wametakiwa kujituma na kulitangaza vyema jina la  Zanzibar wawapo nje ya mipaka ya nchi.

Changamoto hiyo imetolewa leo katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar na Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni,Utalii an Michezo, Bihindi Hamad Khamis, wakati alipowaaga wasanii hao wanaoeelekea nchi za  Lebanon na Misri, kushiriki katika Tamasha la muziki ‘Spring Festival’ litakalodumu kwa muda wa siku tano.


Jumla ya wasanii 11 wa kikundi cha taarabu cha Tausi, kinachoundwa na akinamama watupu wanashiriki katika tamasha hilo, chini ya ufadhili wa vituo vya vya sanaa vya SHAMS ya Beirut na Moreld cha nchini Misri.

Bihindi alisema Serikali ya Zanzibar ina fahari kubwa kuwa na kikundi cha taarabu cha akinamama watupu, kinachopiga muziki katika kiwango cha juu, kiasi cha kupata mialiko kutoka nchi zinazotajika na waanzilishi za muziki huo.

Aliwataka wasanii hao kudumisha nidhamu katika kipindi chote wawapo ughaibuni.

Hii ni mara ya kwanza kwa kikundi hicho kupata mualiko wa kuzitembelea nchi za Mashariki ya Kati, wakati ambapo mwaka 2010 ilipata mwaliko wa kushiriki katika ufunguzi wa mkutano wa  AU mjini Nairobi,Kenya.

Katika tamasha hilo nchi mbali mbali kutoka Bara la ulaya , Mashariki ya Kati na Afrika zinashiriki katika tamasha hilo, zikiwemo Uingereza,Uholanzi,Ujerumani, Tajikistan,Syria,Iran, Misri na Lebanon.

 Wasanii walioondoka kwa safari hio ni pamoja na Mariam Hamdan (kiongozi wa msafara), Mohammed Ilyas, Sheria Issa, Asha Khatibu, Topsy Surrie, Wahida Mohammed, Mwaka Mshindo, Tabu Makame, Tatu Khamis, Fatma Bakar na Fatma bint Baraka ‘Bikidude’.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.