Na Abdi Shamnah
WADAU wa Utalii kutoka sekta binafsi,
wameishauri Serikali kuongeza maradufu bajeti ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar,
ili iweze kujitangaza vyema katika soko la utalii na kufikia dhana ya Zanzibar
kuwa kituo bora cha utalii Duniani.
Wakizungumza na Waziri wa Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk, katika ukumbi wa Hoteli ya
Bwawani jana, wadau hao wamesema Bajeti
ya Kamisheni hiyo kwa mwaka ni ndogo mno kiasi ambacho haitoi taswira kuwa
Serikali inalipa uzito unaostahili suala la kukuza Utalii.
Hii ni mara ya kwanza kwa Waziri
Mbarouk kukutana na wadau hao kutoka taasisi za ZATI na ZATO pamoja na Mameneja
wa Hoteli mbali mbali za kitalii hapa Zanzibar na kupata fursa ya kubadilishana
uzoefu, tangu alipoteuliwa kushika wadhifa wa kuwa Waziri wa Wizara hiyo inayohusika na Utalii.
Walisema Zanzibar ina nafasi kubwa ya
kujitangaza katika soko la Utalii Duniani na kupata mafanikio makubwa kama
ilivyo Mauritius na baadhi ya nchi zilizo katika ukanda wa Mashariki ya Afrika, pindipo itatenga bajeti kubwa katika
kujitangaza kupitia masoko mbali mbali.
Walisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na
vivutio vizuri zaidi ya Mauritius, lakini nchi hiyo imepata mafanikio makubwa
baada ya kutenga bajeti kubwa ya kujitangaza na kuimarisha miundo mbinu yake ya
kiutalii.
‘Mauritius hutenga bajeti ya US Dolla
Milioni 26 kwa mwaka ,wakati bajeti ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar ni
T.Shilingi Milioni 225 tu, hii haionyeshi kuwa Serikali iko ‘serious’ katika dhamira ya
kukuza utalii, alisema meneja wa Hoteli ya Blue bay.
Mapema, akielezea dhima waliyonayo
wekezaji katika Sekta ya utalii Zanzibar, Mkurugenzi Mtendaji wa ZATI Julia Bishop, alisema tayari kuna mafanikio
yaliokwisha kupatikana katika maendeleo ya utalii, ikiwemo uhifadhi wa maeneo ya vivutio vya
utalii, kuongeza mitaji na kupunguza umasikini kwa jamii.
Alisema kuwepo kwa matamasha ikiwemo
lile la Sauti za Busara lililofanyika mapema mwaka huu (February), limesaidia
sana kuongeza idadi ya ujio wa watalii hapa nchini.
Hata hivyo alisema mbali na mafanikio
hayo pia kuna changamoto kadhaa zinazokwaza maendeleo ya sekta hiyo, na
kuyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na utaratibu usioeleweka wa
ukusanyaji wa mapato, usalama wa wageni, vifaa duni na kuwepo urasimu katika
uwanja wa ndege, vizuizi vingi vya Polisi na bughudha za mapapasi kuingilia kazi
za watembeza watalii.
Akitoa nasaha zake, Waziri Mbarouk
aliwahakikishia wadau hao kuwa Serikali imeupokea na itaufanyia kazi ushauri
wote uliotolewa ili kufikia lengo la kuimarisha utalii na kukuza uchumi wa
nchi.
Alisema katika kufanikisha dhana hiyo
anakusudia kuwa karibu sana na wadau hao na kuahidi kukutana nao kila baada ya
miezi mitatu ili kuona kunakuwepo ushirikiano wa kutosha baina ya Serikali na
wadau wa sekta binafsi.
Nae Mshauri maalum wa Rais katika
mambo ya Utalii, Issa Mohammed, alimhakikishia Waziri Mbarouk kuwa wadau hao kutoka sekta binafsi watashirikiana
vyema na Serikali, ili kufikia dhana ya ‘utalii kwa wote’.
Wakati huo
huo Waziri wa Habari, utamaduni ,utalii na michezo, Said Ali Mbarouk
akifuatana
na Balozi mdogo wa Oman aliopo Zanzibar Mansour Al Busaid, jana walitembelea na
kukagua maeneo mbali mbali ambapo Oman inalenga kuisaidia Zanzibar, ikiwa ni
utekelezaji wa makubaliano yaliotiwa saini kati ya nchi hiyo na Zanzibar
“momerundum of understandng’ Agost 17, 2010.
Miongoni mwa
maeno hayo ni pamoja na makumbusho mawili yaliopo Mnazimmoja, Beit el Ajaib,
Makaburi ya ukoo wa kifalme Forodhani pamoja na gofu la Maruhubi Palace.
Hatua hiyo
inalenga kuyafanyia matengenezo majengo ii kuyarejesha katika hali yake ya
asili na kuendeleza uhifadhi wa historia, kwa lengo la kuendeleza utalii.
No comments:
Post a Comment