Habari za Punde

Manispaa Zanzibar Kutumia Bilioni 4

Na Hafsa Golo

MADIWANI katika mji wa Zanzibar limepitisha makadirio ya bajeti ya shilingi bilioni 4.669 yatakayotumiwa na Baraza la Manispaa kwa mwaka wa fedha 2012/ 2013.

Akisoma taarifa ya bajeti hiyo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya fedha ya Baraza la Manispaa, Salma Ibada alisema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 1.936 zitatumika kwa ajili ya mishahara na maposho kwa wanaostahili.

Akichanganua matumizi hayo alisema shilingi milioni 156,383,050 watachangiwa wafanyakazi katika mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ZSSF zikiwa ni asilimia 10 ambayo inapaswa itolewe na muajiri.

Makamu huyo alisema shilingi milioni 369 zitatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo na shilingi bilioni 2.207 zitatumika katika kazi za kawaida.

Makamu huyo alisema kuwa bajeti hiyo imezingatia vipaumbele kadhaa ikiwemo kuimarisha huduma za jamii sambamba na kuendeleza suali la mipango miji.

Akichangia makadirio hayo mjumbe wa Baraza la Madiwani, Mussa Haji Idrissa (CCM) alisema kuwa bajeti hiyo ni finyu kwa mahitaji ya Baraza hilo kwani hasa kutokana na hali ya kupanda kwa huduma za jamii.

Kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa Madiwani kwenye jengo la Baraza la Manispaa mjini hapa, kilihudhuriwa na Meya wa Manispaa ya Zanzibar, Mstahiki Khatib Abrahman Khatib.

Meya huyo alisema atahakikisha kuwa majukumu na wajibu wa Manispaa pamoja na changamoto mbali mbali walizonazo zinasimamiwa ipasavyo kwa mujibu wa kanuni, sheria na kwa amani na utulivu.

Akizungumzia mambo ambayo anatarajia kuyashughulikia katika kipindi cha kwaka wa fedha 2012/2013 ni kuhakikisha sera ya serikali za mitaa inakamilika na kutekelezeka ipasavyo, kuendelea kuimarisha uhusiano wa udugu wa ndani na nje ya nchi kwa mashirikiano na Idara ya Mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa.

Pia kuimarisha mapato ya Manispaa kwa kuanzisha vitega uchumi vikuu kwa mashirikiano na Mabenki, Makampuni binafsi kwa njia za ubia na kutumia uhusiano wa miji iliyopo, kuhakikisha mapato ya vianzio vikuu vya Manispaa vilivyopo serikali kuu vinarejeshwa au vinatumika moja kwa moja katika kuendeleza huduma endelevu za Manispaa.

Naye Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Rashid Ali Juma alisema kwa kuzingatia hali halisi ya mapato na matumizi ya Manispaa itaweza kufikiwa endapo patakuwepo na ushirikiano mzuri katika utendaji.

Alisema gharama kubwa za kuendesha huduma za miji zinatokana na kupanda bei za mafuta, gharama za matengenezo na huduma za magari ya taka, kupunguzwa kwa ruzuku ya serikali katika kuchangia malipo ya mishahara ya wafanyakazi kwa kila mwezi na kulazimika kuchangia mapungufu ya mishahara ya wafanyakazi na kupanda viwango vya mishahara mipya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.