Habari za Punde

Wengi Hawapendi Kuchunguzwa Kongosho- Waziri

WIZARA ya Afya Zanzibar imewataka wanaume kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa kongosho dume ili kuepuka kupatwa na maradhi ya kuziba kwa mkojo.

Waziri wa Wizara hiyo, Juma Duni Haji aliwambia Wawakilishi katika kikao kinachoendelea barazani, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Mpendae, Mohammed Said Mohammed Dimwa.

Mwakilishi huyo alitaka kujua Wizara hiyo inawasaidia vipi wanaume wenye umri mkubwa ili kubaini kama wamepatwa na maradhi ya saratani ya Kongosho dume ili kupatiwa matibabi ya haraka.

Waziri huyo alisema kikawaida wanaume waliofikia umri wa miaka 40 wanatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa Kongosho dume mara moja kwa mwaka ili kumuepusha na tatizo la kuziba kwa njia ya mkojo.

Alisema Zanzibar hivi sasa haina utaratibu maalum wa kuwachunguz wanaume kwa hiari yao, ila wale ambao huenda hospitali kwa matatizo ya kuziba kwa njia ya mkojo na ndipo huonekana kuwa na ugonjwa huo.

Alisema ugonjwa huo mara nyingi huwafanya wanaume kushindwa kupata haja ndogo na iomara nyingi wanaume kupenda kupima tatizo, zaidi ya pale wanapouguwa.

“Si aghalabu wanaume kukubali kupimwa kongosho kabla ya tatizo la kuziba mkojo halijajitokeza na likijitokea kwa taklifu kubwa na ni kwa sababu tu hana jinsi ya kufanya” Alisema Waziri huyo.

Alisema kinachosababisha wanaume kutopenda kupimwa tatizo hilo ni namna ya kipimo kinachotumika kuchunguza maradhi hayo ambacho huhitaji vipimo vyote vya kidaktari ili aweze kujitosheleza na utafiti wake.

Akitaja vipimo hivyo Waziri Duni alisema ni pamoja na kutumia mkono kushika sehemu husika, vipimo vya vyombo maalum vikiwemo X-ray na kupitisha kipimo cha kongosho sehemu ya haja kubwa kwa vile ndiko linakokaa tatizo hilo.

Kutokana na vipimo hivyo, Waziri Duni alisema wengi wa wanaume wamekuwa wakikimbia matibabu hayo na hurudi wakiwa amezidiwa.

Waziri huyo alisema ikiwa wanaume wataendelea kukataa kufuata ushauri huo, wapo hatarini kukumbwa na maradhi ya saratani ya Kongosho kwa sababu ya mabadiliko yatatokea ndani yake.

Akizungumzia juu ya opresheni iliyofanya kuchunguza saratani ya matiti alisema zoezi hilo lilipata mafanikio makubwa baada ya kujitokeza watu wengi na kati ya hao wanne walibainika kuwa na dalili za ugonjwa huo na sita walifanyiwa upasuaji kwa vile ilikuwa ni kubwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.