Na Mwantanga Ame
JESHI la Polisi limeshusha timu mpya ya wapelelezi kwa
ajili ya kuwasaka watu wanaodaiwa kuhusika kuanzisha vurumai iliyodumu kwa siku
mbili katika mji wa Zanzibar.
Hatua hiyo ya Jeshi la Polisi, imekuja baada ya watu
wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar,
(JUMIKI) kuanzisha vurugu ili kutaka kujua hatma ya kiongozi wao aliyekuwa akishikiliwa
na Jeshi la Polisi hilo
katika kituo cha Mwembe Madema.
Kutokana na hali hiyo tayari Jeshi la Polisi,
limeshawakamata watu 76 ambapo kati ya hao 73 wameshafikishwa Mahakamani hadi
mchana wa jana na watatu wanaendelea kufanyiwa uchunguzi ili kukamilishiwa
upelelezi.
Vurugu hizo zilisababisha kuzuka kwa vitendo vya uchomaji
wa moto katika makanisa nyumba ya mlinzi kanisa la Welezo, Nyumba ya Mlinzi ya
Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Baa ya Mbawala, Mzushi na uporaji wa vitu mbali
mbali.
Huku jumuiya ya UAMSHO ikihusishwa kuwa chanzo cha matukio
hayo, wakuu wa Jumuiya hiyo wamekanusha matukio na kudai kufanya vitendo
vilivyofanywa ni kwenda kinyume na misingi ya dini ya kiislamu ambayo inakataza
kufanyika kwa hujuma.
Mkuu wa Jeshi la Polisi, (IGP) Said Mwema, akizungumza na viongozi
wa Makanisa ya Zanzibar na Tanzania bara
katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) la
Kariakoo, wilaya ya
Mjini Unguja, alisema tayari Jeshi la Polisi limeshaongeza wapelelezi kwa ajili
ya kuifanya kazi hiyo.
IGP Mwema, alisema wameamua kuongeza wachunguzi kwa lengo
la kubaini wahusika wa matukio ya uchomaji wa makanisa na vurugu nyengine
kutokana na kuonekana vitendo hivyo ni venye kushabihiana na mambo muelekeo
mwengine.
Alisema walichokibaini katika tukio la mwishoni mwa wiki
baadhi ya watu wameamua kutumia mwanya huo kuendeleza vurugu hizo kwa kuanzisha
maslahi yao binafsi kwa vile wanaofanya hujuma
hizo huondoka na mali
katika maeneo wanayoyashambulia.
“Tumeongeza timu ya wapelelezi kutoka Makao Makuu ya
upelelezi wapo hapa Zanzibari ili kuweza kubaini wahusika na kuwafikisha mbele
ya vyombo vya sheria, tujenge imani watafanya kazi vizuri ila tunaomba muwape
msaada”, Alisema IGP Mwema.
Alisema Jeshi hilo
la Polisi litahakikisha linawatia mikononi wahalifu wote na litawakamata popote
walipo na kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zao.
Alisema katika utekelezaji wa mpango hivi sasa kwa makusudi
Jeshi la Polisi limeamua kuyapa ulinzi makanisa yote baada ya kuorodheshwa
ikiwa ni hatua ya kudhibiti vitendo hivyo.
Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,
Mohammed Aboud Mohammed, akitoa maelezo ya serikali, alisema imesikitishwa na
vitendo vilivyotokea na kuwataka waumini wa kikiristo kutochukua visasi
kulipiza vurugu hizo.
Waziri Aboud, alisema katika kulifanyia kazi suala hilo kuanzia sasa
serikali inapiga marufuku kufanyika kwa mihadhara ya dini, maandamano ambayo
itakuwa haina kibali ha serikali na itakuwa tayari kuwashusha majukwaani
wataokadi kutii amri hiyo.
Alisema nia ya serikali ni kuona inajenga uchumi ulioimara
kutokana na hivi sasa kumekuwa na matatizo mbali mbali ya kukosema ajira kwa
vijana wengi na huduma za kijamii jambo ambalo utatuzi wake utapatikana ikiwa
nchi itabakia katika amani.
Alisema haoni sababu ya matukio hayo kuanza kutokea kwa
mambo hayo wakati miaka ya nyuma Waislamu na Wakristo wa Zanzibar walikuwa kitu kimoja katika mambo
mbali mbali ya shughuli za kijamii.
Aboud, alisema kinachojitokeza sasa kinaonekana kuna jambo
lililojifichwa kwenye ncha ya baadhi ya makundi ambayo yanawapa shaka za
kisiasa na kidini kwa kutumia watu ambao wanaukali wa maisha.
“Haiwezekani mtu tunasema Sheikh anaeaminika kisha aende
kubeba kreti ya bia akimbie nalo serikali itapambana nao naomba nitoe salamu za
pole kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein jambo hili linatusikitisha serikali
nzima”, alisema Aboud.
Aidha, Waziri Aboud, alivitaka vikundi vya dini kuchagua
kazi moja ya kuifanya na sio kuchangaya siasa na dini kwani serikali kwa muda
mrefu imekuwa ikiwaacha kufanya hivyo kwa kutanua demokrasia lakini imeonekana
baadhi ya watu hawako tayari kufanya hivyo kwa amani.
Waziri Aboud, alikiri kwa serikali kufanya kosa kuacha
kuyafanyia kazi masuala hayo wakati yakianza kujitokeza lakini kuanzia sasa
itahakikisha inayadhibiti yasitokee tena.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Abdalla Mwinyi Khamis, akitoa maelezo
yake alisema serikali ya Mkoa itahakikisha inarudisha hali ya amani kwani
vurugu zilizojitokeza hazikuwa ni wazo wala nia ama msimamo wa Mkoa huo.
Nae Mjumbe kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Nauman
Juma Jongo, alisema wameshangazwa na mambo yaliotokea kwani bado yanawapa wasi
wasi kama yalishabihiana moja kwa moja na
mambo ya dini kwani yalihusisha hadi uvunjaji wa maskani za vyama vya siasa na
uchomaji wa bendera.
“Kuna watu wamekunywa bia na kuiba vitu huu sio uislamu, Ofisi
ya Mufti inalaani kitendo hicho lazima tukae kuliangalia vyombo vya usalama
lifanyieni kazi kwa niaba ya waislamu tunawapa pole jamani”, alisema Sheikh
huyo.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Jimbo la Zanzibar Dickson P. Kagaga, aliwataka waumini
wa kikristo kutulia na wasiwaze kulipa kisasi kwani wanaamini kilichotokea
hakitokani na mawazo ya Mzee Abeid Amani Karume.
Hata hivyo, askofu huyo aliiomba serikali kuona inafanya
kazi ya ziada kwa kuyapa ulinzi wa kutosha makanisa yao ili vitendo hivyo visiweze kujirejea
jambo ambalo litaweza kuwatia hasira waumini wa dini hiyo.
Akisoma taarifa ya jumla ya matukio hayo katibu Mkuu wa
Makanisa ya Pentecost Tanzania, Askofu David Andulile, alisema ni vyema kwa
viongozi wa serikali kuona wanachukua tahadhari kwa kuhakikisha sheria inafuata
mkondo wake kwa wataobainika kufanya vitendo hivyo ili kuweza kujenga imani kwa
waumini wao.
Nae Askofu wa Kanisa la Angikana Zanzibar, Michael Hafidh, akitoa maelezo yake
aliiomba serikali kufikiria kuirejesha Kamati ya Amani ili kuweza kushughulikia
matatizo ya aina hiyo.
Nae Askofu wa Kanisa la Roman Catholic Zanzibar, Agostino Shayo, alisema kurudishwa
kwa kamati ya Amani ni jambo la msingi kwa hivi sasa kwani haiwezekani nchi kukosa
kuwa na chombo hicho kwani hapo awali kiliweza kufanya vizuri.
IGP, Mwema bado yupo kisiwani Zanzibar,
kulifanyia kazi suala hilo
ambapo leo wanatarajiwa kukutana na viongozi wengine wa dini.
Mh. Aboud, unasema mtakua tayari kumshusha jukwaani kiongozi wa dini atakaekaidi amri ya kutofanya mihadhara bila kibali.
ReplyDeleteMimi naomba msimshushe kama biharusi, akitoka hapo, aelekee mnazi mmoja!
"Al-himaru..laa, yamshi illa bil aswa"