Habari za Punde

Ofisi za Makamu wa Rais Zaeleza Mikakati yake


Na Rajab Mkasaba, Ikulu
OFISI ya Makamu wa Kwanza wa Rais  wa Zanzibar wamepongeza juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein za kuhakikisha masuala ya Mazingira, UKIMWI, Dawa za kulevya na Watu Wenye Ulemavu yanashughulikiwa kikamilifu na Serikali pamoja na jamii kwa ujumla.

Uongozi wa Ofisi hiyo, ulieleza hayo katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa kuangalia robo tatu ya utekelezaji wa Bajeti  ya mwaka wa fedha 2011-2012 na kulinganisha na robo  ya kwanza na ya pili pamoja na vipaumbele na malengo kwa mwaka wa fedha 2012-2013.


Mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar uliongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ambao pia, ulihudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.

Uongozi huo, ulieleza kuwa umekuwa ukishuhudia kuona Dk. Shein akiwa ameshika usukani katika kutoa mwamko wa masuala ya UKIMWI, dawa za kulevya, masuala ya watu wenye ulemavu na mazingira kiasi ambacho kila akizungumza na wananchi masuala hayo huwa anayagusia.

Waziri wa Wizara hiyo Fatma Fereji, akisoma utangulizi wa taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi, alisema kuwa juhudi za Dk. Shein ndizo zinazoupelekea uongozi wa Ofisi hiyo kuwa na msukumo na hamasa katika kufanikisha malengo waliyojiwekea.

Ofisi hiyo ilimuahidi Dk. Shein kuwa itaendelea kumuunga mkono katika kufanikisha juhudi hizo ili Zanzibar kuwa bila dawa za kulevya, na kuwa mfano katika uhifadhi wa mazingira, udhibiti wa maambukizi mapya ya UKIMWI na kuwa na jamii jumuishi.

Miongoni mwa vipaumbele ilivyoeleza Ofizi hiyo ni pamoja na kuandaa Sera ya Dawa za Kulevya na Sera ya Watu Wenye Ulemavu, kuanza ujenzi wa kituo cha tiba na kurekebisha tabia kwa watu walioacha dawa za kulevya sanjari na kuingiza somo la dawa za kulevya katika mitaala ya skuli.

Nae Makamu wa Kwanza  wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad alitoa pongezi kwa Ofisi hiyo ambayo iko chini yake na kueleza kuwa mafanikio iliyoyapata yanatokana na mashirikiano ya pamoja ya uongozi wa Ofisi hiyo.

Dk. Shein kwa upande wake, alitoa pongezi kwa Wizara hiyo kwa mafanikio iliyoyapata katika utekelezaji wa Mpango kazi wake na kusisitiza haja ya kuwaeleza wananchi mafanikio hayo sambamba na mikakati na mipango iliyowekwa na Idara, Taasisi zake kupitia vyombo vya habari.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwepo kwa kumbukumbu pamoja na umuhimu wa kuandaa ripoti kwa viongozi na watendaji wangine pale wanapofanya ziara za kikazi ndani ya Zanzibar na hata nje ya nchi.

Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambapo Ofisi hiyo katika taarifa yake ilieleza kuwa Dira yake kubwa ni kuwa na Serikali yenye kutoa huduma bora kwa jamii na yenye muhimili mzuri wa uchumi, umoja na maendeleo endelevu.

Sambamba na kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali katika sekta zote za SMZ na mambo ya Muungano kwa kufuatia misingi ya Katiba, Sheria na taratibu pamoja na kuhakikisha kufuata misingi ya haki za binadaamu na ushirikishwaji.

Akisoma utangulizi wa taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi, waziri wa Wizara hiyo Mohamed Aboud Mohamed  imeelezea vipaumbele vyake ikiwa ni pamoja na kuimarisha Kiwanda cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuyafanyia matengenezo majengo ya Kiwanda kilichopo Maruhubi na kununua mitambo mipya kwa ajili ya kiwanda hicho.

Aidha, Ofisi kwa kushirikiana na COSTECH na wadau wengine itaendelea kuimarisha shughuli za utafiti kwa kuainisha vipaumbele vya utafiti, kujenga uwezo Kamati za kusimamia masuala ya utafiti, kuwajengenea uwezo watafiti chipukizi pamoja na kutafuta fedha kwa ajili ya shughuli za utafiti.

Kwa vile nchi inakabiliwa na sherehe kubwa za maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ofisi imeeleza kuwa imeweka kipaumbele kwa matayarisho ikiwemo ununuzi wa vifaa, na kuandaa mpango mzima wa maadhimisho hayo.

Pia, Ofisi hiyo imeweka kipaumbele katika kuendelea kujenga uwezo wa jamii juu ya kukabiliana na maafa kwa kutoa elimu, kutafuta vifaa, kuazisha vituo vya dharura na kuandaa  majaribio ya kujiandaa na maafa.

Nae Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa Ofisi hiyo kwa mafanikio iliyoyapata pamoja na mashirikiano yaliopelekea kupata mafanikio hayo huku akisisitiza haja ya kwuaeleza wananchi juu ya mafanikio hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.