Na Khamisuu Abdallah
KUFUATIA fujo zilizotokea juzi katika mji wa Zanzibar na vitongoji
vyake, kumepelekea kusita kwa baadhi ya huduma za elimu katika baadhi ya skuli
mbalimbali za mjini Unguja.
Zanzibar Leo ilishuhudia baadhi ya skuli hizo kusimamisha
masomo kutokana na vurugu zilizoanza Jumamosi na hivyo baadhi ya skuli za mjini
hapa kuwaondosha mapema wanafunzi kabla ya kukamiika kwa viipindi vya masomo.
Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya skuli zilizositisha
masomo hayo kuwa ni pamoja na skuli za Mwanakwerekwe, Darajabovu, Kajificheni
na skuli za mjini.
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Mwanakwerekwe “H” Hityari Haidhuru
Ramadhan, akizungumzia kadhia hiyo alisema wameamua kusitisha huduma hizo
kutokana na fujohizo kwani zinawapa wasiwasi mkubwa wa kuendelea na masomo hasa
ikizingatiwa kuwa wanafunzi wanaweza kudhurika na fujo hizo kwa njia moja au
nyengine.
Alisema pamoja na mambo mengine wameamua kusitisha masomo
kutokana na skuli hiyo kuwepo karibu na Mahakama ya Wilaya Mwanakwerekwe,
ambapo watuhumiwa wa fujo hizo wamekuwa wakipelekwa mahakamani hapo kujibu
tuhuma zinazowakabili.
“Wanafunzi waliohudhuria skuli hapo inawapelekea kutoka
madarasani na badala yake kutizama askari waliokuwepo nje ya mahakama hiyo hali
ambayo inayowazidisha wasiwasi kwa wanafunzi hao,” alisema mwalimu mkuu huyo.
Sambamba na hilo,
Mwalimu Hityari, alisema kutokana na
fujo hizo kumekuwa na mahudhurio madogo ya wanafunzi skulini hapo ambapo wazazi
wamekuwa wakizuia watoto wao.
“Tumewasiliana na Afisa wa Elimu Wilaya kuwa hali sio nzuri
katika maeneo ya Mwanakwerekwe na hivyo tukatakiwa kuwaondosha wanafunzi mapema
pamoja na sisi walimu na hali hii si kwa leo tu tutaendelea na utaratibu huu
hali itapotulia ,” alisema Mwalimu huyo.
Hivyo mwalimu huyo aliwataka wazazi kuwazuia watoto wao
hadi hapo hali itakaporejea kama kawaida, kwa
lengo la kuepusha madhara yatakayoweza kutokea.
Kwa upande wa wazazi wa wanafunzi ambao hawakutaka kutajwa
majina yao,
walisema wamesikitishwa na vitendo vinavyofanywa na wanaosadikiwa wafuasi wa
jumuiya ya muamsho.
Walisema vitendo hivyo kwa kiasi kikubwa vimekuwa
vikirejesha nyuma kuwaruhusu watoto wao kwenda maskuli na hata wao kuendelea na
kazi zao za ujenzi wa taifa.
Aidha waliwataka watu walioanzisha fujo hizo kuacha mara
moja kwani kufanya hivyo kunapelekea kuzorotesha huduma mbalimbali za kijamii
na kuifanya nchi kutokuwa na amani.
Wazazi hao waliiomba serikali kudhibiti vitendo hivyo na
kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaohusika na vitendo vya uvunjifu wa
amani katika kisiwa cha Unguja.
No comments:
Post a Comment