Habari za Punde

Aukacha ukurugenzi ufundi, Ataka Uraisi

Aukacha ukurugenzi ufundi, ataka uraisi

Na Aboud Mahmoud

MWANASOKA mkongwe hapa Zanzibar Salum Bausi Nassor, ameitupilia mbali ofa ya Mkurugenzi wa Ufundi aliyopewa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).

Bausi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa timu ya Wazee Sports, ameliambia gazeti hili kuwa, hana haja na nafasi hiyo ambayo hivi karibuni, Makamu wa Rais wa ZFA Haji Ameir Haji, alitangaza kuwa amepewa mwanasoka huyo veterani.

Ameir alitoa taarifa hiyo kupitia kipindi cha michezo kinachorushwa na televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).

Bausi ametaja sababu zilizomfanya alikatae fupa hilo, kuwa ni pamoja na kuwa hana elimu ya kiwango cha stashahada yaani ‘Diploma’, ambayo alisema ni miongoni mwa sifa muhimu kwa mtu anayepewa wadhifa wa Mkurugenzi wa Ufundi.

Sababu nyengine alisema, ni dhamira yake ya kuwania uraisi wa ZFA kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Rais wa zamani wa chama hicho Ali Ferej Tamim, ambayo tayari ameisema hadharani.

“Mimi ninataka uraisi wa ZFA, sina haja ya ukurugenzi, tayari nimeshatangaza nia ya kuchukua fomu za kugombea kiti hicho, najiandaa kwa hilo, hivyo ni vyema nafasi hiyo apewe mtu mwengine”, alisisitiza mchezaji huyo wa zamani wa Black Fighters, Miembeni na Zanzibar Heroes.

“Mkurugenzi wa Ufundi ni lazima awe uwe na diploma ya soka kama aliyonayo Sunday Kayuni wa TFF, mimi nina ‘advance’ tu, vipi nipewe kazi hiyo”, alifahamisha.

Aidha alihoji kwa nini ZFA ione sasa haja ya kumpa nafasi hiyo, baada ya kutanganza kuwa anataka kugombea uraisi, naye yupo siku nyingi na hakufikiriwa kabla kwa ukurugenzi huo.

Alifahamisha kuwa, endapo atapata ridhaa ya wapiga kura, lengo lake kuu ni kuinua soka la Zanzibar akishirikiana na viongozi wenzake pamoja na wadau mbalimbali wa mchezo huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.