Habari za Punde

Super Falcon Yaota Kung'ara Kimataifa


Yapania kuiondolea Zanzibar aibu ya kichwa cha kichaa

Na Haji Nassor, Pemba

BAADA ya kupata uhakikia wa asilimia 99 kutwaa ubingwa wa soka Zanzibar, uongozi wa timu ya Super Falcon umeanza kupata ndoto za kuiletea Zanzibar ushindi katika mashindano ya kimataifa mwakani.

Uongozi huo umesema kuwa utahakikisha unaimarisha kikosi chake kabla ya kuingia kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika na ile ya Kombe la Kagame kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, ili kufuta aibu ya Zanzibar kuwa ngazi ya timu nyengine kubeba mataji.

Akizungumza kwenye uwanja wa Gombani mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa kuhitimisha ligi kuu ya Zanzibar kwa kuifunga Kikwajuni magoli 5-0, Rais wa klabu hiyo Hafidh Suleiman, alisema ili kutimiza lengo hilo, ni lazima waongeze nguvu kwa kutafuta wanasoka wa ziada walio mahiri na uzoefu.

Alisema pamoja na ukweli kwamba wachezaji walionao sasa ndio walioipa ushindi timu hiyo, lakini kwa vile imekabiliwa na mashindano ya kimataifa, hawana budi kuongeza wachezaji ili kuimarisha baadhi ya idara ikiwemo ya ushambuliaji.

Hata hivyo, Rais huyo ameomba sapoti ya wadau wa soka wa Zanzibar, pamoja na kuwataka wahudhurie kwa wingi kila timu hiyo itakaposhuka dimbani kupepesuha bendera ya nchi.

"Lazima Wazanzibari na hasa wapenda soka, wahakikishe wanatuunga mkono na kutupa nguvu za hali na mali, ili kukiimarisha kikosi chetu na kuwapa hamasa wachezaji na viongozi, ili waweze kufanya vyema kwenye mashindano ya kimataifa", alishauri Rais huyo.

Akizungumzia shutuma kwamba waliwanunua wachezaji wa Kikwajuni ili wafunge magoli mengi, Suleiman alikanusha vikali madai hayo, matokeo hayo ni sawa na mengine ambapo timu hufungwa idadi kubwa ya magoli.

"Hata hao Kikwajuni ambao wameshuka daraja, ndani ya msimu huu waliwafunga KMKM idadi kama hiyo ya magoli, Simba juzi imeifunga Yanga magoli 5-0, je wamenunua? Mbona watu hawasemi hayo?", alihoji kwa mshangao.

Alisema kamwe hawakununua mchezo huo, bali walicheza kwa nguvu zao pamoja na Kikwajuni kujitahidi lakini waliizidi ujanja na kuibuka na ushindi huo mnono.

Timu ya Super Falcon ambayo ilipanda daraja la ligi kuu msimu huu, imemaliza michezo yake na kufikisha pointi 39, na kabla ya mchezo wa Jamhuri dhidi ya Kikwajuni keshokutwa, imejiweka katika nafasi inayoipa uhakika wa ubingwa kwa asilimia kubwa kutokana na akiba nzuri ya magoli ya kufunga iliyonayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.