Habari za Punde

Watakaojifungua Hospitali za Serikali Kutotozwa Ada - Dk Shen

 Na Rajab Mksaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ametangaza kuwa huduma za uzazi kwa akina mama wajawazito wanaokwenda kujifungua katika hospitali za umma Unguja na Pemba zitafanyika bure. 

 Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Tunguu, wakati alipokuwa akitowa majumuisho ya ziara yake ya siku tatu aliyoifanya katika Mkoa wa Kusini Unguja na kusisitiza kuwa huduma hizo hazitolipiwa tena. 

 Katika maelezo yake, Dk. Shein amesema kuwa hatua hiyo ni pamoja na kuondosha ada kwa akina mama wajawazito wanaokwenda kujifungua katika hospitali zote za Serikali ikiwemo hospitali kuu ya Mnazi Mmoja. 


 Alisisitiza kuwa haiwezekani na hakuna sababu ya msingi ya kuwachangisha akina mama wajawazito Shilingi arobaini elfu kwa ajili ya kupata huduma ya kujifungua. Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haiwezi kushindwa kuchangia mchango huo kwa akina mama wajawazito kwani mchango huo hauna tija kwa serikali na wala sio mchango wenye kiasi kikubwa cha fedha.

 Alisema kuwa hoja kubwa ni kupunguza matatizo ya wazazi wanayopata wakati wa kujifuangua ikiwemo vifo, huku Serikali ikiwa na lengo la kufikia Milenia katika sekta ya afya, hivyo imeamua kwa makusudi kutowatoza fedha akina mama hao na fedha zote italipa serikali yenyewe.

 “Hivyo niulize ndugu zangu tukiwaambia wazazi wachange elfu arobaini ndio tunawasaidia hivyo?...... mimi nimeamua hili tuliondoshe kabisa”,alisisitiza Dk. Shein, 

 Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kina mama wote ni lazima watambue hilo na Serikali itatilia mkazo na mwaka huu itaongeza fedha za dawa, vifaa ili huduma ziweze kuimarika na kupunguza utegemezi kutoka kwa wahisani. 

 Dk. Shein ameeleza kuwa imefika wakati Zanzibar ianze kujitegemea na kuepuka kukaa pembeni na kuwasubiri wahisani kwani kuna siku wanaweza kusema hawana na badala yake kusababisha hali kuwa mbaya zaidi. 

 “Ni vizuri tuanze wenyewe, tusisubiri wahisani, hivi sasa tumefika pazuri kutokana na hali yetu ya uchumi ilivyo…..Zanzibar tunakopesheka kwa kiasi kikubwa kwani uwezo upo”,alisema Dk. Shein. 

 Akieleza ombi alilopewa na wakulima wa bonde la mpunga la Muyuni B, la kutaka wapatiwe kinu cha kusagia mpunga, alisema kuwa serikali haishindwi na kueleza kuwa tayari ameshamuagizia Katibu Mkuu Wizara ya kilimo kutafuta kinu kilichobora na madhubuti ambacho kitadumu muda mrefu na kueleza kuwa hata yeye anawaeza kununua kinu hicho kwa fedha zake mwenyewe. 

 Akieleza matatizo ya ardhi yaliomo katika Mkoa huo, Dk. Shein alirejea kauli yake ya kuwataka viongozi wa Mkoa kuimaliza wenyewe migogoro ya ardhi na kusema kuwa huo sio utawala Bora, iwapo Kamati ya Maendeleo na Wilaya hazifahamiani katika kutatua tatizo hilo. 

 “Nakueleza kuwa iwapo nitalimaliza mwenyewe kama mlivyotaka itakuwa kazi imekushindeni na mtakuwa hamfai, na iwapo mkiifanya wenyewe nitakupeni pongezi na zawadi….Hili kalifanyeni wenyewe ili mvuke na hayo mengine yasitokee”alisisitiza Dk. Shein. 

 Alieleza kuwa matatizo ya Chwaka na Uroa hayana tija na alimpongeza Dk. Mwinyihaji Haji Makame ambaye ni Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na wenziwe na kueleza kuwa hiyo ni hatua kubwa, na vizuri tukakutana kila mara ili kuepuka kutotokea tena hali hiyo. 

 Ni muhimu viongozi kuwa karibu na wananchi tunaowatumikia na tunaowaongoza pamoja na kuwasilikiza wanacho sema na wanachowaambia viongozi wao na kuwatanabahisha viongozi kuwasimamia wananchi wao bila ya kujali itikadi ya kisiasa, dini wala ukabila.

 Dk. Shein aliendelea kusisitiza hali ya amani na utulivu na kueleza kuwa iwapo hali hizo hazitokuwepo kutapelekea maendeleo kuwa duni na wawekezaji pamoja na hata watalii wanaokuja kuitembelea na kuekeza Zanzibar hawatakuja.

 Alisisitiza kuwa amani iliyopo Zanzibar haitovunjwa na itabakia kama ilivyo kwani watu wake wameihangaika kuitafuta amani hivyo kwa muda mrefu hivyo Wazanzibari hawatakuwa tayari nchi yao kurejeshwa ilikotoka 

 Alieleza kuwa Zanzibar imefika pahala pazuri katika kuiongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa kwa maendeleo ya nchi na wananchi wake na ndani ya serikali hiyo viongozi wote wamekuwa na mashirikiano makubwa. 

 Nao uongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja ulimpongea Rais kwa ziara yake hiyo ambayo aliifanya katika Mkoa huo na kueleza kuwa imewapa somo na changamoto kubwa katika kufanikisha kazi zao za kila sikuna kuahidi kutekeleza yake yote aliyoyaagiza katika majumuisho hayo na yale aliyoyaagiza katika ziara yake hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.