Yadai timu haikupiga mwamuzi, yamtosa mchezaji
Na Ameir Khalid
SIKU mbili baada ya timu ya soka ya JKU kutwangwa adhabu na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kutokana na mchezaji wake kumpiga mwamuzi, wajenga uchumi hao wamedai hawakustahiki kuadhibiwa kama timu.
JKU imetozwa faini ya shilingi laki mbili na ZFA Taifa, sambamba na mchezaji wake Khamis Kombo Faki kufungiwa mwaka mmoja na kupigwa faini ya shilingi laki moja kwa hatia ya kumpiga kichwa mwamuzi Issa Haji Vuai, wakati timu hiyo ilipocheza na Mtende Rangers Aprili 26, mwaka huu katika uwanja wa Dimani.
Kutokana na kutoridhishwa na maamuzi hayo, uongozi wa timu hiyo umeamua kukata rufaa katika Kamati ya Rufaa na Usuluhishi ya ZFA Taifa kutaka ibatilishe maamuzi hayo, kwa madai kuwa kitendo cha mchezaji kumpiga mwamuzi, hakiihusu timu kwani haikumtuma kufanya hivyo.
Barua ya JKU ya tarehe 2 Mei, 2012 iliyotumwa katika kamati hiyo, imefahamisha kuwa, hata mchezaji huyo amehukumiwa kinyume na kifungu cha kanuni ya ZFA namba 12 kuhusu faulu na utovu wa nidhamu, ambacho kinafafanua viwango vya adhabu kwa mchezaji anayetenda kosa la kupinga maamuzi ya mwamuzi, kwamba huadhibiwa kwa kuoneshwa kadi ya njano.
Aidha, imeeleza kuwa kama mchezaji huyo ataendelea kutenda kitendo hicho, anapaswa kuoneshwa kadi ya pili ya njano ambayo itakuwa sawa na nyekundu na hivyo ndivyo ilivyotokea.
Maelezo ya uongozi huo, yamefafanua zaidi kuwa, JKU kama timu, hakustahiki kuadhibiwa na ndio maana adhabu zote zilizotolewa na mwamuzi huyo, alizielekeza wa mchezaji mwenyewe, na sio mashabiki wala timu yake.
Iliongeza kuwa hata wachezaji wa timu hiyo walisaidia kumtoa mwenzao baada ya kuoneshwa kadi nyekundu, lakini aliwaponyoka na kurudi uwanjani ambako alimpiga kichwa mwamuzi huyo.
Katika kuonesha kutokuhusika kwake na kitendo cha kupiga, timu hiyo ilisema ilichukua uamuzi wa kumtibu mwamuzi huyo ambaye alipasuka kutokana na kupigwa huko, pamoja na kumuhakikishia usalama wake uwanjani hapo.
"Hakuna kiongozi, mwanachama wala shabiki wa timu ya JKU ambao kwa pamoja wanaounda timu hiyo aliyehusika na kosa la kukataa maamuzi ya mwamuzi, na hivyo tunapinga adhabu iliyotolewa na ZFA katika kifungu cha 16 (d)", ilisema sehemu ya barua hiyo.
Mbali na kuiruka adhabu hiyo, JKU pia imepinga hatua ya kuipa ushindi timu ya Mtende Rangers, ambao umeifanya ipande daraja la ligi kuu msimu ujao.
No comments:
Post a Comment