Habari za Punde

Ligi Zanzibar Yafika Patamu

Na Asya Hassan

MATOKEO ya sare ya 2-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya soka Zanzibar kati ya timu ya Zimamoto na Jamhuri juzi, yamezidi kukizonga kitendawili cha timu itakayotwaa ubingwa msimu huu.

Pambano hilo lililochezwa uwanja wa Amaan, lilikuwa la kasi na ushindani mkubwa hasa ikizingatiwa timu zote mbili zina nafasi ya ama kunyakua ubingwa au angalau kushika nafasi ya pili itakayowawezesha kuiwakilisha Zanzibar kwenye mashindano ya kimataifa mwakani.

Jamhuri ambayo ni makamu bingwa wa msimu uliopita, ilikuwa ya kwanza kuzifumania nyavu za wapinzani wao kwa goli murua lililofungwa na mchezaji wake machachari Ali Othman katika dakika ya sita.

Bao hilo liliwazindua waokozi wa majanga na wazima moto wa mtaa wa Kilimani, na kuanza kuliandama lango la Jamhuri kwa mashambulizi ya nguvu kutafuta bao la kusawazisha.

Jitihada hizo zilizaa matunda mnamo dakika ya 30 ambalo liliwekwa kimiani na Hamid Mgeni, na timu hizo kwenda mapumziko zikiwa zimefungana bao 1-1.

Mabadiliko kadhaa ya wachezaji yaliyowafanywa na timu zote katika kipindi cha pili, yalizidisha hamasa na kasi ya mchezo hali ilitotoa burudani mwanana kwa watazamaji waliojimwaga uwanjani hapo kushuhudia wanaume hao wakiumana.

Zimamoto iliweza kuzichana tena nyavu za Jamhuri katika dakika ya 76 lililopachikwa na Khatib Said na kuiweka Jamhuri katika wakati mgumu,

Hata hivyo, huku baadhi ya mashabiki wa Jamhuri wakionekana kukata tamaa, mchezaji Suleiman Ali alifanikiwa kubadilisha matokeo alipomudu kuisawazishia timu yake mnamo dakika ya 80.

Kwa matokeo hayo, Jamhuri imefikisha pointi 36 ikiwa imebakiwa na mchezo mmoja dhidi ya Kikwajuni, huku sare hiyo ikiitimizia Zimamoto pointi 31 na michezo miwili mkononi dhidi ya Mundu inayotapia roho kubaki ligi kuu, na ule wa Mafunzo.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo Mafunzo, nao bado wamo katika resi za kuwania taji licha ya kuwepo katika nafasi ya sita, kwani hadi sasa wamejikusanyia pointi 27, na kubakiwa na michezo mitatu ambayo kama itashinda yote, itafikisha pointi 36 ambazo tayari Jamhuri inazo huku ikibakiwa na mchezo mmoja

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.