UCHAGUZI mdogo kujaza nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Wilaya ya Magharibi, unatarajiwa kufanyika Mei 20, mwaka huu.
Kufanyika kwa uchaguzi huo kunafuatia agizo la ZFA Taifa, baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama wilayani humo Shaaban Juma, aliyeachia ngazi mwishoni mwa mwaka jana.
Tayari chama hicho kimeunda kamati ya watu watano kushughulikia uchaguzi huo tangu hatua za awali hadi utakapofanyika, ambayo inaongozwa na Issa Ahmada Hija akiwa Mwenyekiti.
Wengine katika kamati hiyo ni Abdallah Bakari Abdallah anayekuwa Katibu, Rashid Suleiman, Mshika Fedha pamoja na wajumbe wawili, Seif Sanani Seif na Othman Babu Jomo.
Katibu wa kamati hiyo Abdallah Bakari Abdallah, alisema fomu kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo zinaanza kutolewa leo katika ofisi za chama wilayani humo zilizoko Mwanakwerekwe, na kwamba mwisho wa kuzirejesha ni Mei 11, siku ambayo pia wagombea watafanyiwa usaili.
Bakari amesema wanachama wa ZFA Wilaya ya Magharibi ambao ni viongozi wa klabu zote kuanzia daraja la tatu, ndio watakaopiga kura kuchagua Mwenyekiti mpya.
Akizungumzia uchaguzi huo, Mwenyekiti wa kamati hiyo Issa Ahmada Hija, aliwahakikishia wapiga kura na wagombea wote watakaoteuliwa kuwania kiti hicho, kuwa kamati yake itafanya uadilifu kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki ili kuepusha malalamiko.
Alitoa wito kwa wanamichezo wote kujitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo iliyobaki wazi tangu Oktoba 7, mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment