Korti yairejesha Malindi ligi kuu Zanzibar
ZFA yadai Malindi si mwanachama wake
Na Salum Vuai, Maelezo
ANGA la mchezo wa mpira wa miguu Zanzibar, limeendelea kutawaliwa na amri za mahakama ambako baadhi ya klabu zimekimbilia kuomba shufaa kwa kutoridhika na maamuzi ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).
Hatua ya hivi karibuni, inaihusu klabu ya soka kongwe hapa nchini Malindi SC, ambayo mahakama ya Mkoa wa Mjini Magharibi Vuga, imeamuru irejeshwe katika Ligi Kuu msimu wa 2012/13.
Kwa mujibu wa barua ya mahakama hiyo ya jana tarehe 18, Mei, 2012 iliyotumwa kwa ZFA Taifa, yenye nambari ya kumbukumbu MMK/82/2012, ZFA imetakiwa kuirejesha timu hiyo katika ligi kuu ili kutekeleza uamuzi uliotolewa na mahakama ya Mkoa Vuga Zanzibar mbele ya Hakimu wa Mkoa Dhamana, Hamisa Suleiman Hemed.
Barua inayoigiza ZFA itekeleza amri hiyo, imeambatanishwa pia na waraka wa dikrii inayofafanua madai ya Malindi iliyowasilisha mbele ya mahakama hiyo mwaka jana, kupinga hatua ya ZFA kuishusha daraja, ambapo ilidai kuwa haikufuata kanuni na katiba ya chama hicho.
Miongoni mwa madai ya timu hiyo wakati huo, ilikuwa kuzuia ligi kuu isichezwe hadi pale itakapopata haki yake, ambapo baadae yalifikiwa makubaliano kwa masharti kwamba pande hizo zitekeleze mambo ya msingi ili Malindi iweze kucheza ligi hiyo msimu uliopita.
Aidha, Malindi ilitaka ilipwe fidia ya shilingi milioni 30, kufidia gharama ilizodai imeingia kwa ajili ya kujiandaa na ligi ambapo ushiriki wake ulifutwa na ZFA, hali iliyoilazimisha iamue kupanda ngazi za mahakama kutafuta haki.
Imeelezwa kuwa, Malindi inapaswa kushiriki ligi kuu msimu ujao, huku nayo ikitakiwa ikamilishe taratibu za kuiwezesha kucheza katika ligi hiyo.
Hukumu hiyo ya mahakama huenda ikaiweka ZFA katika wakati mgumu kwani tayari imeshapata timu mbili Mtende Rangers na Duma zilizopanda daraja kutoka la kwanza hadi ligi kuu ijayo, huku timu ya tatu ikitarajiwa kujulikana baada ya mechi mbli maalumu kati ya timu za Hard Rock na Bandari.
Aidha, ligi hiyo inayotarajiwa kuanza mwezi wa Agosti, imepata mdhamini kinywaji cha Grand Malt ambaye tayari ameshasaini mkataba wa kugharamia ligi akitambua kuwa inashirikisha timu 12 tu.
Alipoulizwa Ofisa Habari wa ZFA Munir Zakaria, alisema chama chake hakitambui amri hiyo ya mahakama kwa sababu kimsingi Malindi si miongoni mwa wanachama wake.
Alieleza kwa mujibu wa marekebisho ya dharura ya katiba ya ZFA yaliyofanywa mwishoni mwa mwaka jana, klabu yoyote itakayofungua kesi mahakamani kuhusiana na soka inakuwa imejifuta yenyewe uanachama na hivyo, na kuitaka Malindi isipoteze muda.
Alieleza kushangazwa na hukumu hiyo, akidai kuwa ZFA haikuitwa mahakamani na kuhoji ni vipi mahakama hiyo itoe maamuzi bila kuwepo mshtakiwa.
No comments:
Post a Comment