Wadau Pemba waitetea Kikwajuni
Wadai imegeuzwa kitambaa kufuta uchafu ZFA
Na Masanja Mabula, Pemba
ADHABU iliyotolewa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Taifa Pemba dhidi ya timu ya soka ya Kikwajuni, imezua jambo miongoni mwa wadau wa soka kisiwani Pemba, ambapo baadhi yao, wamesema imetolewa kwa nidhamu ya woga.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tafauti, wadau hao wa michezo wamesema, adhabu hiyo kwa klabu ya Kikwajuni ni njia ya kujisafisha kutokana na uendeshaji mbovu wa ligi ya msimu uliopita ambao umefanywa na ZFA, wakisema ilikamilika kwa mizengwe.
Wamedai kuwa, hata baadhi ya vifungu vilivyotumiwa na chama hicho kuiadhibu Kikwajuni, haviendani na adhabu hiyo ambayo wamesisitiza kuwa Kikwajuni imegeuzwa kitambaa cha kufutia uchafu wa ZFA ili ionekane haikuhusika na uendeshaji ligi usiozingatia kanuni na taratibu za kisheria.
Wamedai ZFA imetumia kifungu namba 18 (a) (i) na (ii) inayozungumzia makosa ya kuchafua, kuvuruga mchezo au kupanga matokeo kwa makusudi kwa kujichelewesha, kupunguza idadi ya wachezaji, kujifungisha, kujipatia idadi ya magoli ya kupeana kwa makusudi katika mazingira yanayotia shaka timu zote zitafutiwa matokeo.
Hata hivyo, wameeleza kushangazwa kwao na hatua ya ZFA kuiadhibu Kikwajuni pekee bila kuangalia upande wa pili ambao ni timu au watu walioshirikiana na timu hiyo kupanga matokeo.
"Kwa kweli adhabu hii haikutendea haki Kikwajuni, kwani kama amepanga matokeo, bila shaka alishirikiana na upande mwengine, ambao ZFA imeufumbia macho", alieleza Khamis Faki.
Aliongeza kuwa, kifungu namba (a) (ii) cha kanuni hiyo ya 18, kinasema kuwa, ikiwa viongozi, walimu, wachezaji, au kamisaa wameshirki kuvuruga, kuchafua na kupanga matokeo watafungiwa mwaka mmoja pamoja na faini ya shilingi laki moja kila mmoja, na kusema kuwa si kamisaa wala upande ulioshirikiana na Kikwajuni kufikia hali hiyo ulioadhibiwa.
Aidha alisema adhabu za aiana hiyo zinafaa ziwe zinachukuliwa kwa timu yeyote ile kwani tumeshuhudia baadhi ya Timu zinazoshiriki ligi hiyo zikishindwa kufika kwenye vituo kwa ajili ya michezo na ZFA ilikaa kimya bila ya kuchukua hatua kama hiyo .
Kwa upande wake, Meneja wa timu ya Jamuhuri Mohammed Abeid 'Elisha', aliishauri ZFA iwe makini katika maamuzi yake na kuitaka izingatie sheria na kanuni za kuendesha mpira wa miguu badala ya kufanya mambo kwa utashi au maslahi binafsi.
Amedai, kuiadhibu Kikwajuni kwa kuishusha madaraja mawili, kuifungia kucheza kwa miaka miwili sambamba na kuiga faini ya shilingi milioni moja na laki mbili, hakutoshi kuonesha uwajibikaji wa ZFA wala ufuatiliaji wake wa kanuni na sheria za chama hicho.
Mmoja wa viongozi wa ZFA Taifa Pemba (jina tunalo), alisema kuwa chama hicho kimetoa adhabu hiyo kwa kuzingatia kanuni za kuendesha mashindano na kwamba hakijakurupuka katika kutumia vifungu hivyo kuiadhibu Kikwajuni, ambayo nayo imesema haitakaa kimya na itapanda ngazi zote husika ili kutafuta haki.
No comments:
Post a Comment