Na Asya Hassan
TIMU ya SS Lazio ya Chumbuni imefanikiwa kunyakua mbuzi, seti ya jezi na mipira miwili baada ya kuibuka bingwa katika ligi ya jimbo la Chumbuni, 'Khamis Guu Cup', iliyokuwa ikifanyika kwenye uwanja wa skuli ya Chumbuni.
Ubingwa huo umekuja baada ya Lazio kuishinda Kiboiza kwa changamoto ya mikwaju ya penelti, kufuatia wanaume hao kushindwa kufungana kwenye muda wa kawaida.
Hata hivyo, ushindi huo haukuja kirahisi, kwani miamba hiyo ilijikuta ikifikisha penelti nane hadi Lazio ilipomudu kushinda pale wapinzani wao walipopoteza mkwaju wa mwisho na wao kumaliza udhia kwa kupachika nyavuni.
Mgeni rasmi katika mchezo huo, Mwakilishi wa jimbo la Chumbuni Machano Othman Said aliyechangia jezi na mipira vyenye thamani ya shilingi 832,000, alikabidhi zawadi hizo kwa washindi.
No comments:
Post a Comment