Habari za Punde

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif akutana na Balozi wa Msumbiji.


Na Hassan Hamad. (OMKR)
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inaendelea na juhudi zake za kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nchi za nje.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alipokuwa na mazungumzo na balozi wa Msumbuji nchini Tanzania Bw. Amour Zacaria Kupela huko Ofisini kwake Migombani.

Amesema katika jitihada hizo serikali inakusudia kumwagilia jumla ya ekari elfu nane ambapo hadi sasa imefanikiwa kumwagilia ekari elfu mbili chini ya ufadhili wa serikali ya Korea.

Maalim Seif amefahamisha kuwa tayari washirika wengine wa maendeleo wameshaonesha nia ya kushirikiana na Zanzibar katika kilimo hicho cha umwagiliaji, na kwamba iwapo azma hiyo itakamilika Zanzibar itapunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa chakula.

Sambamba na hilo Makamu wa Kwanza wa Rais amesema serikali pia inaimarisha utafiti wa kilimo na mbegu ili kupata mbegu bora ambazo baadaye zitasambazwa kwa wakulima kwa ajili ya kuendeleza kilimo.

Kwa upande mwengine amesema serikali bado inaendelea na mikakati ya kupunguza tatizo la ajira kwa vijana kwa kutoa elimu ya mafunzo ya amali ili vijana waweze kujiajiri pale wanapomaliza masomo yao.

“Serikali imeanzisha Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika kwa lengo la kupunguza tatizo la ajira ingawaje wapo vijana waliomaliza vyuo vikuu bado hawana ajira”, alifahamisha.

Maalim Seif amefafanua kuwa tatizo hilo linatokana na vijana wengi kusomea masomo ambayo yana wataalamu wa kutosha, na kutoa wito kwa vijana kutafuta masomo yatakayowawezesha kujiajiri baada ya kuhitimu.

Akizungumzia kuhusu suala la maji, Maalim Seif amesema Zanzibar bado inakabiliwa na tatizo hilo kutokana na uchakavu wa miundombinu ya maji pamoja na upungufu wa maji kwenye vianzio unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Hata hivyo amesema serikali tayari inalijua tatizo na imo katika mikakati ya kuliondosha.
Kuhusu mafanikio ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Maalim Seif amesema mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na kuendelea kwa amani na utulivu, hali inayovutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza Zanzibar.

Kwa upande wake balozi huyo wa Msumbiji anayemaliza muda wake Bw. Amour Kupela, amepongeza hatua iliyochukuliwa na Zanzibar ya kufikia maridhiano ya kisiasa na kupelekea kuundwa kwa serikali ya Umoja wa kitaifa ambayo inaonyesaha kupata mafanikio makubwa.

Balozi Kupela ameongeza kuwa Msumbiji na Zanzibar zina uhusiano wa kindugu wa muda mrefu na kutaka uhusiano huo uendelezwe kwa maslahi ya pande hizo mbili.

Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais amekutana na uongozi wa Jumuiya ya Muzdalifat inayoyojishughulisha na utunzaji wa mayatima, pamoja na watoto wanaotarajia kusafiri kuelekea nchini Uturuki.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo sheikh Abdallah Hadhir Abdallah amesema watoto hao wanne wanakwenda nchini Uturuki kwa ajili ya kushiriki katika kongamano la kimatifa kuhusu maadhimisho ya siku ya watoto yatima linalotarajiwa kufanyika mjini Istambul Uturuki kuanzia tarehe 28 mwezi huu hadi tarehe 3 mwezi ujao.

Watoto hao Salum Ali Mohd (miaka 10), Hajir Khalid Haji (miaka 11), Shufaa Mohd Ali (miaka 12) na Lutfia Sheha Mussa (miaka 11) wataongozana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Muzdalifat Sheikh Abdalla Hadhir, Katibu wa Jumuiya ustadh Farouq Hamad Khamis na Mkuu wa kitengo cha mayatima Zanzibar Nassra Suleiman Abdallah.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.