Miembeni United yaiuzia Mundu daraja
Yaelezwa ni hatua kuitwaa nafasi hiyo
Na Salum Vuai, Maelezo
KLABU ya soka ya Miembeni United imevunjwa rasmi jana na uongozi wake kuamua kuuza daraja la Ligi Kuu kwa timu ya Mundu iliyoshuka daraja katika msimu uliomalizika Ijumaa iliyopita.
Hafla ya kuuziana daraja hilo ilifanyika jana katika ukumbi wa kituo cha Elimu Mbadala Rahaleo mjini hapa, ambapo kila timu iliwakilishwa na viongozi wake wa juu pamoja na mawakili wao.
Mmoja wa waliokuwa viongozi wa Miembeni United Haji Sultan Tembe (Haji Kaka), amelithibitishia gazeti hili kuwa, klabu hiyo imevunjwa rasmi na wachezaji wake wako huru kusajiliwa na timu yoyote.
“Ni kweli tumeamua kuachana na mambo ya soka ili tuangalie shughuli nyengine baada ya kuona mpira wa miguu Zanzibar hauna tija yoyote”, alieleza.
Naye Katibu wa klabu ya Mundu Mussa Diku, alikiri kuwa wamenunua nafasi ya Miembeni United na baada ya makubaliano hayo yaliyosainiwa jana, taratibu nyengine zitafuata ili kuiwezesha timu hiyo kucheza ligi kuu msimu ujao.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, hatua hiyo inalenga kumpa nafasi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Miembeni United kabla kuvunjwa jana Amani Ibrahim Makungu, kugombea uraisi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).
Chanzo chetu cha uhakika kutoka mamlaka za juu za michezo nchini, kimethibitisha kuwa, mipango ya chinichini inasukwa kumuandaa Makungu kushika nafasi ya uraisi wa ZFA iliyobaki wazi kufuatia kujiuzulu kwa Ali Ferej Tamim Aprili 2, mwaka huu.
“Ni kweli Makungu amekuwa akipigiwa debe hata na baadhi ya viongozi wa serikali, ili agombee, lakini kwanza anatakiwa asiwe kiongozi wa timu yoyote, kuiuza timu yake nadhani ni hatua muhimu”, kilifafanua chanzo hicho kwa sharti la kutokutajwa jina.
Zanzibar Leo ilimtafuta Makungu kwa njia ya simu, ambaye alisema anafahamu kuwepo ushawishi huo kutoka kwa mamlaka na wadau mbalimbali wa mjini na vijijini, lakini kwa sasa hayuko tayari kuzungumza kwa undani kama atagombea au hapana.
“Miembeni United tumeiuza kwa sababu nyengine za ndani, lakini sio kwa kuwa nataka uraisi wa ZFA, ingawa ninaweza kuwania kiti hicho kama hao wanaotaka niingie tutafikia muafaka wa namna ninavyokusudia kukibadilisha chama hicho kimaendeleo”, alifafanua.
Mwezi mmoja na nusu umepita tangu Ali Ferej Tamim alipojiuzulu uraisi wa ZFA, na kutoa nafasi ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo kujaza kiti hicho, ndani ya miezi mitatu kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
No comments:
Post a Comment