Na Haroub Hussein
MASHINDANO ya soka kuwania kombe la Jihad, yamefikia tamati kwa timu ya Sayari kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kbaada ya kuichapa Taifa jipya kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 5-2.
Katika pambano hilo lililofanyika juzi uwanja wa Amaan, ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, miamba hiyo ilimaliza dakika 90 ikiwa sare ya 2-2 na kulazimika kuhukumiana kwa matuta.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Mwakilishi wa jimbo la Magogoni Abdilahi Jihad Hassan, yalishirikisha timu tisa za jimbo hilo.
Akifunga michunuano hiyo, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, alisema serikali inaendelea na juhudi za kuirejeshea Zanzibar hadhi ya kimichezo ambayo iliifanya itambulike hata nje ya nchi.
Hata hivyo alisema, ili kufikia hatua hiyo, kunahitajika ushirikiano wa kutosha kati ya vyama vya michezo, Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) na serikali, na kueleza kuwa bila ya hivyo hakuna jambo jema litakalofanyika.
Amesisitiza kuwa, ili michezo ipige hatua, ni lazima vyama na wadau waachwe malumbano kwani wote wana dhamira ya kujenga nyumba moja, hivyo wasaidiane mawazo ya kurekebisha kasoro badala ya kulumbana.
Aidha alipongeza hatua ya kuanzishwa mashindano hayo, akisema utaratibu kama huo ni muhimu katika kuwaondolea vijana mawazo yasiyokuwa na manufaa, na pia kuwafanya washirikiane kuleta maendeleo badala ya kubaguana kwa misingi ya vyama vyao.
Katika hatua nyengine, alisema ili kukuza mchezo wa mpira wa miguu, ni vyema chama husika kijipange vyema kuepuka matatizo mbalimbali yanayochangia kudumaza maendeleo ya soka Zanzibar.
Alihitimisha kwa kuwataka vijana wa jimbo hilo kujitahidi katika michezo, akisema mbali na kuimarisha afya, pia ni njia mojawapo ya kujipatia ajira kupitia sekta hiyo.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Mwakilishi wa jimbo la Magogoni na mdhamini wa mashindano hayo Abdilahi Jihad Hassan, aliwataka Wanamagogoni kujipanga katika sekta ya michezo ili waweze kutoa wachezaji mbalimbali katika timu za Taifa kwa maendeleo yao.
No comments:
Post a Comment