Habari za Punde

Simba yawasili Mjini Khartoum Sudan

Na Ezekiel Kamwaga, Khartoum

TIMU ya soka ya Simba imewasili salama jijini Khartoum, Sudan juzi saa 5:49 ikitokea jijini Nairobi, Kenya tayari kwa pambano lake la marudiano la Kombe la Shirikisho (CAF) dhidi ya Al Ahly Shandy.

Msafara huo wa Simba wenye wachezaji 19 na viongozi wanane, umefikia katika hoteli ya Shariqa, lakini jana ilitarajiwa kwenda katika mji wa Shandy uliopo umbali wa kilomita 150 kutoka Khartoum.

Mechi kati ya timu hizo imepangwa kurindima keshokutwa saa mbili usiku katika uwanja wa Shandy wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 10,000.

Msafara wa Simba ulilakiwa na uongozi wa Chama cha Soka cha Sudan (SFA) lakini ukajikuta ukiwekwa uwanjani hapo kuanzia saa 6:00 hadi 7:30 usiku, kwa kisingizio cha kumalizika taratibu za kiulinzi na kiusalama uwanjani hapo.

Alipoulizwa sababu za kucheleweshwa huko hadi usiku wa manane, kiongozi mmoja wa SFA alijibu kwa mkato kuwa, “Hata kwenu pia mlifanya hivihivi.”

Simba inatarajiwa kuanza mazoezi leo usiku, baada ya mapumziko ya siku nzima. Timu hiyo pekee ya Tanzania iliyobaki kwenye mashindano ya kimataifa, na ilishinda mchezo wa kwanza dhidi ya Al Ahly Shandy kwa mabao 3-0.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.