Wanawake Unguja wapongezwa kwa ujasiriamali
Na Laylat Khalfan
WANAWAKE kisiwani Unguja, wamepongezwa kujitokeza kwao kwa wimgi na kujiunga na Jumuiya ya wajasiriamali na masoko Zanzibar.
Afisa tawala Mkoa Kusini Unguja, Juma Hamad, alitoa pongezi hizo, huko Tunguu katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kusini Unguja, wakati akifungua mkutano wa jumuiya ya wajasiriamali na masoko Zanzibar, kutokana na mafanikio waliyoyapata tangu kujiunga na jumuiya hiyo.
Alisema ni jambo la kupigiwa mfano kwa kuwaona wanawake wanahitaji maendeleo na kuondokana na fikra ya kuwa mwanamke ni ni mama wa familia asiyeweza kujiletea mabadiliko ya kiuchumi pekee pasi na kushirikishwa wanaume.
“Wanawake mzidi kusonga mbele katika kujiletea maendeleo na sio kuwategemea akina baba hali hii itarudisha nyuma maendeleo yenu”, alisema Afisa tawala.
Aidha aliwataka wanawake wasijiweke nyuma kielimu bali wawe tayari kufuata kikamilifu taaluma wanayopatiwa na wataalamu ili wapate manufaa zaidi ya kiuchumi pamoja na familia zao.
Hata hivyo, aliwataka wajasiriamali hao kutotosheka na ufugaji wa wanyama tu bali pia wajishirikishe na kilimo cha muda mfupi kama vile mbogamboga ambapo wataweza kupata msukumo imara wa kiuchumi.
“Wakati umefika kwa jamii yetu mnatakiwa mubadilike kwa kwenda na wakati kwa kulima kwa kufuata wataalamu wa kilimo, kwa kuelekezwa namna ya kulima kilimo cha utaalamu zaidi na kupata mazao yenye kiwango bora na kuleta faraja katika uchumi wetu ”, alisema.
Alisema katika kilimo pia wanaweza kupata manufaa ikiwa ni pamoja na kuuza bidhaa ambapo kipato kitawasaidia katika familia na kuendleza shughuli zao za ufugaji.
No comments:
Post a Comment