KITANDAWILI cha Rais mpya wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kinatarajiwa kufumbuliwa Juni 30, mwaka huu siku ambayo chama hicho kimetangaza kuwa ndiyo utakapofanyika uchaguzi mdogo kujaza nafasi hiyo.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa akikalia kiti hicho Ali Ferej Tamim, tangu Aprili 2, 2012.
Ofisa Habari wa ZFA Munir Zakaria, amefahamisha kuwa, kamati tendaji ya ZFA itakutana kabla ya kumalizika wiki hii pamoja na kamati ya uchaguzi iliyo chini ya Mwenyekiti Gulam Abdallah Rashid kujadili mambo muhimu kuhusiana na uchaguzi huo.
Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa, ni pamoja na kupanga tarehe za kuchukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi hiyo, sambamba na siku ya kuwafanyia usaili wagombea watakaopitishwa.
Katika hatua nyengine, Zakaria amesema chama hicho kimeunda kamati ya kutafuta fedha kwa ajili ya kusaidia ushiriki wa timu ya Taifa ‘Zanzibar Heroes’ katika mashindano ya kombe la dunia kwa nchi zisizokuwa wanachama wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) yaliyopangwa kufanyika katika nchi ya Kurdistan kuanzia Juni 4, mwaka huu.
Kamati hiyo ya watu saba inaongozwa na Munir Zakaria (Mwenyekiti), Katibu ni Kassim Haji Salum, Masoud Attai (Mshika Fedha), ambapo wajumbe ni Abdallah Thabit, Laila Said na Asaa Khamis.
Zakaria amewaomba wadau mbalimbali, taasisi za umma na binafsi, kuiunga mkono timu hiyo kwa kuichangia vitu mbalimbali ikiwemo fedha na vifaa ili iweze kupeperusha vyema bendera ya Zanzibar huko Irak.
No comments:
Post a Comment