Habari za Punde

Bandari Yatinga Ligi Kuu Zanzibar.


Na Haji Nassor, Pemba
WAVUTA nanga wa timu ya soka ya Bandari, wameungana na timu za Duma na Mtende Rangers kutinga Ligi Kuu ya Zanzibar kwa msimu ujao wa mwaka 2012/13, baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Hard Rock katika mchezo uliopigwa uwanja wa Gombani juzi.

Mchezo huo ulikuwa wa marudiano kati ya miamba hiyo kufuatia ule wa awali uliochezwa uwanja wa Mao Dzedong wiki kadhaa zilizopita, ambapo wapiga mizinga wa Hard Rock walikubali kipigo cha magoli 2-1.

Katika pambano hilo lililokuwa kali na la kusisimua, Bandari ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuingia katika nyavu za wapinzani wao kwa goli lililofungwa na Mussa Omar ‘Kidishi’ mnamo dakika ya 40, aliyeuwahi mpira uliopigwa na Yussuf Juma na baadae kutemwa na mlinda mlango, akiujaza kimiani kirahisi.

Goli hilo lilidumu hadi mapumziko, na Hard Rock walikianza kipindi cha pili kwa kasi na uchu wa kusaka mabao wakihaha kila sehemu, ingawa walikumbana na ulinzi usiopepesa wa masarahange wa Bandari.

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa Hard Rock kwa kuwapumzisha Ramadhan Said na Ibrahim Khamis na nafasi zao kuchukuliwa na Bakari Suleiman na Bawazir Waziri, yaliwawezesha wapiga mizinga hao kujipatia goli la kusawazisha katika dakika ya 88, ambalo lilipachikwa nyavuni na Salim Mkubwa.

Hata hivyo, Hard Rock ilikuwa imechelewa kwani sare hiyo haikuwa na manufaa yoyote kwake, na hivyo kuipa Bandari tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Grand Malt inayotarajiwa kuanza mnamo mwezi wa Agosti mwaka huu, ikishirikisha timu 12.

Akizungunza na waandishi wa habari baada ya mtanange huo, kocha Hamad Hilika wa Bandari alisema, mchezo huo ulikuwa mgumu lakini alikuwa na uhakika wa kusonga mbele kwa kuwa kikosi chake kilikuwa kimeandaliwa vyema.

Kwa matokeo hayo, timu hiyo pamoja na Mtende Rangers na Duma zilizopanda daraja hivi karibuni, zinakamilisha jumla ya timu 12 zitakazoshiriki ligi msimu ujao.

Timu nyengine ni Super Falcon, Jamhuri, Chipukizi, Mundu (walionunua daraja toka Miembeni United), Miembeni SC, KMKM, Zimamoto, Chuoni pamoja na Mafunzo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.