Habari za Punde

Dk Shein Akutana na Ujumbe wa Wakuu wa Vyuo Vikuu vya China


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Kiongozi wa Ujumbe wa Wakuu wa Vyuo Vikuu vya China, Dk.Jiang Bo,wakati ulipofika Ikulu Mjini Zanzibar kuonana na Rais jana. [Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Ujumbe wa Wakuu wa Vyuo Vikuu vya China, unaongozwa na Dk.Jiang Bo,(wa tatu kushoto) wakati ulipofika Ikulu Mjini Zanzibar kuonana na Rais na kuzumza nao jana. [Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa uhusiano na ushirikiano kati ya China na Zanzibar sasa umezidi kuimarika baada ya China kuonesha azma ya kushirikiana na Zanzibar katika elimu ya Juu kwa kupitia vyuo vyake vikuu vya elimu.

 Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa Wakuu wa Vyuo vya China ukiongozwa na Kiongozi wa Jumuiya ya Elimu ya Mahusiano ya Kimataifa ya China Dk. Jiang Bo uliofuatana pamoja na uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA. 


 Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina historia kubwa ya mashirikiano na uhusiano kati yake na China hatua ambayo imepelekea kupatikana kwa mafaniki makubwa na kueleza kuwa kutokana na vyuo hivyo vya China kuwa vya muda mrefu tokea kuanzishwa kwake ikifananishwa na chuo kikuu cha SUZA, hatua hiyo ya mashirikiano itasaidia. 

 Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa China imeweza kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo elimu na kusisitiza kuwa hatua ya nchi hiyo kuimarisha ushirikiano katika elimu ya juu ni wa kupigiwa mfano.

 Alieleza kuwa mbali ya sekta ya elimu china imeweza kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta kadhaa ikiwemo afya,kilimo pamoja na sekta nyenginezo. Kwa upande wa sekta hiyo ya elimu, Dk. Shein alisema kuwa ujio wa viongozi na wakuu wa vyuo vikuu vya China hapa Zanzibar na kuonesha azma ya kushirikiana na katika sekta ya elimu kupitia Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA, inatoa mwangaza mpya wa maendeleo. 

 Dk. Shein alieleza kufarajika kwake na hatua ya vyuo hivyo kuonesha azma ya mashirikiano kwa kusaini makubaliano ya mashirikiano pamoja na Mkataba wa Mafahamiano na chuo kikuu cha SUZA. Alisema kuwa hatua hiyo inafungua ukurasa mpya wa mashirikiano katika elimu ya juu hali ambayo itasaidia na kupelekea mashirikiano kwa elimu hiyo ya juu na kusisitiza haja kwa mashiriano hayo kwa wakufunzi wa vyuo hivyo vya China kuja kubadilishana uzoefu na ujuzi kati yao na chuo cha SUZA. 

 Alisema kuwa mbali ya mabadilishano hayo ya uzoefu pia, itawasaidia hata wanafunzi wa vyuo hivyo kushirikiana katika suala zima la utafiti na kuweza kubadilishana uzoefu na utaalamu baina ya pande mbili hizo. Dk. Shein pia, aliwaeleza viongozi hao kuwa Zanzibar ni sehemu pekee ambayo imepata mafanikio kwa kusomesha lugha ya kiswahili katika chuo chake kikuu cha SUZA, kutokana na chimbuko la lugha hiyo hapa nchini na kusisitiza kuwa itakuwa ni jambo la busara vyuo hivyo vikawa na ushirikiano katika nyanja hiyo. 

 Nao Wakuu hao wa Vyuo vya China walieleza azma yao ya kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na elimu ya juu kwa kuweza kubadilishana uzoezu pamoja na utaalamu baina ya pande mbili hizo. 

 Walieleza kuwa China inajivunia uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati yake ya Zanzibar hatua ambayo imeweza kuleta mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta za maendeleo. 

 Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Rais wa Chuo Kikuu cha Dalian of Technology Profesa Zhang Dexiang, Mwenyekiti wa Chuo Kikuu cha Shanghai Jiao Tongm Profesa Ma Dexiu,Msaidizi wa Rais wa Chuo Kikuu cha Mianyang Normal na Msaidizi wa Rais wa Chuo Kikuu cha Shangai Jiao Tong vyote vya China.

 Wakuu hao wa vyuo wameleza uhusiano wao mzuri na mashirikiano yaliopo kati ya vyuo vyao hivyo na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA, na kusisitiza kuwa vyuo vyao itauimarisha na kuukuza zaidi kwa manufaa ya pande zote mbili. 

 Walieleza kuwa elimu ni jambo muhimu katika kukuza na kuleta maendeleo endelevu, hivyo juhudi za makusudi kwa mashirikiano ya pamoja zitachukuliwa katika kuhakikisha sekta hiyo inaimarika hapa nchini sanjari na kukuza mafahamiano zaidi kielimu. 

 Walieleza kuwa vyuo vyao vimekuwa na mashirikiano mazuri na Wizara husika ya elimu ya China mwao na kueleza kuwa pia, vimekuwa vikitoa nafasi za masomo kadhaa kwa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania. 

Viongozi hao walieleza kuwa mbali ya nafasi hizo za masomo wanazozitoa pia, wakufunzi wake hupata nafasi za kwenda nje ya nchi hiyo kwa ajili ya kutoa mafunzo ya miezi mitatu mitatu Nae Makamu Mkuu wa Chuo cha SUZA, Profesa Idris Rai, alimueleza Dk. Shein kuwa Chuo Kikuu cha SUZA kimekuwa na uhusiano mwema na vyuo hivyo hatua ambayo imezidi kuimarika kutokana na kusaini Mikataba ya mashirikiano na mafahamiano katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.