Habari za Punde

Kukimbia Kutoa Maoni ni Kujitia Kitanzi- Serikali


SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imewahakikishia wazanzibari kuwa maoni yao hayatatupwa kapuni na badala yake yatafanyiwa kazi na serikali na kuonya kuwa kukimbia kutoa maoni ni sawa na kujitoa kitanzi. Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Sheria ya Katiba Zanzibar, Abubakar Khamis Bakari huko Mapofu Wingwi, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
“Wananchi nakutoweni wasi wasi, maoni yenu hayatachakachuliwa, tume ya kukusanya maoni ina wajumbe sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, kamwe wajumbe wetu hawataisaliti Zanzibar”, alisema Bakari ambaye ni Mwakilishi wa jimbo la Mgogoni.

Bakari alisema anafahamu mawazo ya wazanzibari yalivyo hivi sasa yalivyo juu ya suala la Muungano na namna hisia zao zilivyo lakini aliwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kutoa maoni yao kwani ili yafanyiwe kazi na kuahidi kwamba hakutakuwa na njia yoyote ya kufanyika udanganyifu.
“Nawasihi Wazanzibari tuitumie fursa hii kutoa maoni yetu, ili Zanzibar iwe na uwezo wa kufanya mambo yake kwa maslahi ya Wazanzibari, kukimbia kutoa maoni yetu ni sawa na kujitia kitanzi”, alionya Waziri huyo ambaye kitaalumu ni mwanasheria.
Alisema kwamba tume ya kukusanya maoni itakafika Zanzibar kwa kazi, huo ndio utakuwa wakati mzuri wa kusema kitu gani wanakitaka wazanzibari katika Muungano na kumaliza kasoro ambazo wanaziona ni kero kwao na ni mambo ambayo hayafai kuwa ya Muungano.
Akitoa onyo kwa wazanzibari Bakari alisema kwamba iwapo wananchi hawatajitokeza kutoa maoni, itaonekana wameridhika na mfumo uliopo pamoja na utaratibu wa sasa wa uendeshaji wa Muungano na hivyo kupoteza fursa muhimu ya maslahi ya nchi yao.
Waziri huyo alisema tume hiyo ya kukusanya maoni ya wananchi inayoongozwa na Jaji Warioba inatarajiwa kuja wiki hii kwa ajili ya kuzinduliwa rasmi na kuanza kuchukua maoni ya wananchi juu ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza katika mkutano huo mgeni rasmi wa shughuli hiyo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kwa upande wake amewahimiza Wazanzibari kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa uhuru juu ya aina ya Muungano wanaoutaka, wakati tume ya kuchukua maoni ya wananchi itakapo kuja Zanzibar.
Maalim alisema fursa waliyonayo wananchi kutoa maoni yao katika mchakato wa kuandika Katiba ya Jamhuri ya Mungano ni adhimu na wala wasikubali kuhadaiwa au kutishwa na mtu yeyote na kuipoteza haki yao hiyo.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza wanachama wa CUF na wananchi wengine waliohudhuria katika mkutano wa hadhara kuwa katika miaka 48 ya Muungano wananchi hawajapata fursa kama hiyo, hivyo wasikubali kuitupa, na hasa kwa vile hawana uhakika iwapo itatokea tena katika maisha yao.
Akizungumzia msimamo wake binafsi Maalim Seif alisema ajenda kuu kwa Wazanzibari katika mchakato wa kuandika katika mpya ni Muungano, hasa kwa kuzingatia Zanzibar inayo katiba yake ya mwaka 1984 inayojumuisha mambo mengi yanayowahusu Wazanzibari, kama vile haki za binaadamu, mgawanyo wa madaraka na mambo mengineyo.
Awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma na Haki za Binaadamu wa chama hicho, Salum Bimani aliwapongeza viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa juhudi kubwa wanazozichukua katika kuondoa shida za wananchi.
Alitoa mfano wa juhudi kubwa zilizochukuliwa na ambazo tayari zimeanza kuza matunda na kuwanufaisha wananchi ni kulishughulikia tatizo la usafiri wa baharini kati ya Unguja na Pemba na kupandisha bei ya zao la karafuu.
Bimani alisema wananchi wanapaswa kuwapongeza kwa dhati viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakiwemo Rais Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili, Balozi Seif Ali Iddi kwa juhudi kubwa wanazozichukua kumaliza tataizo la muda mrefu na usafiri kati ya visiwa hivyo.
Ziara hiyo ya Maalim Seif na ujumbe wa chama chake imelenga kukagua uhai wa chama cha CUF, katika majimbo ya Mgogoni na Micheweni ambapo Bimani alisema ziara hiyo imewatambulisha kwamba bado wanachama wa chama hicho wana imani na viongozi wao na wapo tayari kufanya nao kazi kwa ajili ya kuendeleza chama chao.

2 comments:

  1. Sasa kuna ubaya gani kujitoa kitanzi kama mada inavyosema?; ni sawa kujitia kitanzi!?

    ReplyDelete
  2. KAKA, MAKALA HAIJAKAA VIZURI HIYO, SIO KICHWA CHA HABARI WALA BAADHI YA MANENO YA NDANI.

    NENO KUJITIA KITANZI NAONA LIMESUMBUA, LINASOMEKA (KUJITOA KITANZI)

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.