Habari za Punde

Copa Coca Cola Kusini Pemba Yalia njaa

Na Haji Nassor, Pemba
TIMU ya vijana wa chini ya miaka 17 ya Mkoa wa Kusini Pemba, inayojiandaa kwa michuano ya Copa Coca Cola, imepaza kilio chake kinachososababishwa na njaa kwa wachezaji wake.

Timu hiyo imepiga kambi katika uwanja wa michezo Gombani Wilaya ya Chake Chake, ikijinoa kwa ngarambe hizo za kila mwaka zinazoshirikisha timu za mikoa yote ya Tanzania, ambazo zimepangwa kuanza Juni 24 mwaka huu jijini Dar es Salaam na Kibaha mkoani Pwani.

Kocha wa timu hiyo Jongo Juma Jongo, amesema hadi sasa, hakijapokea hata senti moja kutoka kwa wadau wa soka mkoani humo, ikiendelea na matayarisho duni, huku kukiwa hakuna hata kiongozi mmoja aliyewatembelea angalau kuwapa ushauri.

Alieleza kuwa, fedha chache walizopelekewa na wadhamini wa michuano hiyo kampuni ya Coca Cola kwa ajili ya safari, ndizo walizotumia kwa ajili ya kununua chakula cha wachezaji.

"Tulitarajia viongozi wa Mkoa wa Kusini na wapenda michezo wenge watakuwa na hamu ya kutoa misaada kwa timu hii ambayo ni yetu sote, ili ipate matayarisho mazuri na kuiwezesha kusnda ubingwa wa mashindano hayo, lakini hali haiko hivyo", alieleza kwa masikitiko.

Aidha alisema walitaraji kupatiwa angalau msaada wa chakula, maji na dawa lakini mambo yanavyokwenda ni dhahiri yanaweza kuwa sababu kubwa kama watafanya vibaya kwenye michuano hiyo.

Hata hivyo, alisema pamoja na kukosa huduma muhimu kambini, wachezaji wake wanaonesha jitihada kubwa na kwamba wamepania kushindana kwa ajili ya kunyakua ubingwa wa michuano hiyo mwaka huu.

Timu ya mikoa huo ambayo katika mashindano kama hayo mwaka mwaka 2010, iliweza kufika nusu fainali, na mwaka jana kutolewa mapema, inatarajiwa kuondoka Pemba Juni 20 kwenda jijiji Dar es Salaam tayari kwa patashika hizo.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.