Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MCHEZAJI mahiri wa nafasi ya kiungo wa klabu ya Yanga Haruna Niyonzima, amegeuka wakala wa wachezaji, baada ya kuushawishi uongozi wa timu hiyo kumpa ulaji mshambuliaji Meddy Kagere anayemaliza mkataba na timu ya Polisi ya Rwanda.
Niyonzima, aliyepachikwa jina la kiungo-mshambuliaji wa Hispania na Barcelona Fabregas, ambaye alitamba na Yanga msimu uliopita amezungumza na viongozi wa kamati ya usajili ya Yanga, na kuwaambia kuwa Kagere ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na kwamba anaweza kuisaidia sana klabu hiyo msimu ujao.
"Kagere ni mshambuliaji mzuri sana, nimekaa naye timu ya taifa namuona anavyocheza ni aina ya mchezaji ambaye Yanga inastahili kuwa naye", alisema Niyonzima kuliambia gazeti la Mwanaspoti.
"Viongozi wa Yanga wamezungumza naye na mambo yanakwenda vizuri, nadhani tukirudi Rwanda wanaweza kumalizana naye. Ni mchezaji mwenye juhudi sana anayeweza kupunguza tatizo la mabao hapo Yanga, ana juhudi sana halafu si mtu wa kukubali kushindwa kirahisi", aliongeza alipokuwa akizungumza kutoka Nigeria alikokuwa na timu ya Taifa Amavubi.
Alizidi kumsifia kwa kusema iwapo atafanya kazi kwa uwezo wake wote anaojua yeye, Yanga itafika mbali na atang'ara sana na timu hiyo na kwmaba hata kwenye ligi ya Tanzania atakubalika haraka.
Mmoja wa viongozi wa kamati ya usajili ya Yanga, alikiri kuwa Niyonzima amewahakikishia kwamba endapo watamsajili mchezaji huyo watakuwa wameramba dume.
Hata hivyo, aliongeza kuwa bado wanaendelea na mazungumzo ya kupata beki wa kati kutoka kwenye timu ya taifa ya Kenya au Uganda na mkakati mwengine ni kuhakikisha wanamalizana na Kagere ambaye aliwahi kuitolea nje Gor Mahia ya Kenya.
Pamoja na kuwa tayari, washambuliaji wa Yanga Davies Mwape wa Zambia na Kenneth Asamoah wa Ghana wametua jijini Dar es Salaam, timu hiyo imeamua kuachana na wachezaji hao ili kusajili wapya wawili kutoka nje, Kagere akiwa miongoni mwao.
Hadi sasa, Simon Msuva wa Moro United ndiye mshambuliaji pekee mzalendo ambaye Yanga imeshamsajili hadi kwa msimu ujao wa ligi.
No comments:
Post a Comment