Habari za Punde

Makungu, Bausi Wachukua Fomu .

Makungu: Sikupewa shindikizo nimeamua mwenyewe.  


Bausi: Nimesukumwa na kauli ya Dk. Shein kwa ZFA


Na Salum Vuai, Maelezo
KIPYENGA cha mbio za kuwania urais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kimepulizwa jana baada ya wagombea wawili, Amani Ibrahim Makungu na Salum Bausi Nassor kuchukua fomu katika ofisi za Kamati ya Uchaguzi zilizoko uwanja wa Amaan.

Bausi ambaye ni mwanasoka mkongwe na Mwenyekiti wa timu ya Wazee SC, alikuwa wa kwanza kuwasili kwenye ofisi hizo mnamo saa 5:45 asubuhi, akiambatana na kaka yake Seif, Mkurugenzi wa Chama cha Wakulima (AFP) Rashid Yussuf Mchenga na wanamichezo kadhaa wanaomuunga mkono.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa fomu yake, Bausi alisema pamoja na mambo mengine, pia uamuzi wake huo umepata nguvu kutokana na kauli ya Rais wa Zanzibar aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari, kwamba amechoka kusikia malumbano katika ZFA huku soka la Zanzibar likiendelea kudidimia.

Alifahamisha kwamba ana nia ya dhati kuleta mabadiliko na kumfuta machozi Rais Dk. Shein pamoja na wapenda michezo wa Zanzibar, ambao kwa miaka mingi sasa wamevunjwa moyo na hali ya soka la visiwa hivi.

"Naingia katika kinyang'anyiro hicho nikiwa na dhamira ya kweli kuleta mabadiliko, ili Zanzibar irudi kwenye chati, ninawaomba wajumbe wa mkutano mkuu wa ZFA wapime tulikotoka na tulipo sasa, ili tushirikiane katika kuinua kiwango cha soka cha nchi yetu", alisema Bausi.

Alitaja baadhi ya mikakati yake kuwa ni pamoja na kuzijengea mazingira mazuri timu za vijana ili ziwe msingi bora wa timu za taifa na klabu kubwa, kuwainua waamuzi kimaslahi na kuimarisha uwezo wa makocha, kujenga ofisi ya kudumu kwa ZFA, na kutafuta haki za Zanzibar katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kwa upande wake, Makungu alikanusha taarifa zilizoenea mitaani kwamba amesukumwa na baadhi ya viongozi wa serikali kujitosa kwenye uchaguzi huo, na kusema kuwa hayo ni mapenzi yake kwenye mpira wa miguu, na uchungu alionao kwa nchi yake kushindwa kupata maendeleo katika mchezo huo.

"Kwamba mimi nina damu ya michezo hasa soka hakuna asiyefahamu, niligombea umakamu mwaka 2010 nikashinda, lakini yaliyotokea mliyaona, bado nimekuwa na ndoto kwamba siku moja niwe kiongozi wa juu wa ZFA kwa kuleta ufanisi, sikushawishwa wala kubembelezwa na mtu", alifafanua Makungu.

Alisema anaingia kwenye mpambano huo akifahamu fika kuwa, kuongoza ZFA kunahitaji moyo wa kujitolea, na yeye hagombei kwa kufuata maslahi, bali anachotaka ni kuisaidia serikali katika jitihada zake za kuendeleza michezo iiwemo kuinua soka la Zanzibar ambalo kuimarika kwake kunahitaji viongozi makini na wenye upeo na ubunifu wa kutafuta nyenzo.

Alisema iwapo atachaguliwa kukiongoza chama hicho, baadhi ya mambo atakayoyapa umuhimu ni kuhakikisha ZFA inaondokana na aibu ya kupanga ofisi na kutishiwa kuhamishwa kwa kulimbikiza kodi, pamoja na kuunda kamati moja tu itakayoshughulikia kutafuta fedha kwa ajili ya uendeshaji wa timu za taifa, za wanaume, wanawake na vijana, Kombe la Mapinduzi na mashindano mengine mbalimbali.

Uchaguzi wa Rais wa ZFA umepangwa kufanyika Juni 30, kujaza nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Ali Ferej Tamim aliyeachia ngazi Machi 2, mwaka huu 2011 kwa sababu za kiafya na kifamilia, baada ya kukiongoza chama hicho kwa zaidi ya miongo miwili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.