Habari za Punde

Mama Shein, Iddi waibeba Copa Coca Cola Kaskazini


Na Mwantanga Ame
TIMU ya soka ya Mkoa wa Kaskazini Unguja inayojiandaa na mashindano ya Copa Coca Cola, imepigwa jeki na mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein pamoja na Mama Asha Suleiman Iddi, mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Mama Shein na Mama Iddi, wameikabidhi timu hiyo vifaa mbalimbali vya michezo, pamoja na vitu vyengine kwa matumizi ya kambi ya wanasoka hao wanaojinoa kwa ajili ya mashindano hayo yaliyopangwa kuanza Juni 23, mwaka huu mjini Dar es Salaam na Kibaha.

Akisoma risala mbele ya Mama Asha Iddi kabla ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Mjumbe wa kamati ya maandalizi Mosi Ame, alisema kambi hiyo yenye wachezaji 20 na viongozi sita, inakabiliwa na uhaba wa chakula, kitoweo pamoja na wachezaji kukosa viatu na vikinga miguu (shin-guard’ na glovu za magolikipa.

Alisema ingawa baadhi ya viongozi wa Mkoa huo wamejitolea kuisaidia timu hiyo, lakini bado misaada waliyotoa ni midogo na wanahitaji vifaa na mahitaji zaidi ili waweze kufanya vizuri katika michuano hiyo.

“Lengo letu ni kwenda kushindana na sio kushiriki, ili turudi na ushindi mnono na kuupa hadhi mkoa wetu kwa kuinua viwango vya wanamichezo”, alieleza.

Akizungumza kwa niaba ya Mama Shein, mke wa Makamu wa Pili wa Rais Mama Asha Iddi, aliahidi kuwa watajitahidi kuisaidia timu hiyo ili ishiriki vizuri michuano hiyo, wakitambua kuwa michezo ni ajira kwa vijana na utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Aidha aliwataka vijana hao kuendeleza amani ya nchi, na kuacha kujiingiza katika vurugu ambazo alisema zinaweza kuwaletea matatizo yatakayodumaza vipaji vyao.

Vifaa vilivyokabidhiwa kwa timu hiyo, ni jezi seti moja, soksi, sabuni pamoja na kuahidiwa viatu na tiketi kwa ajili ya safari yao ya kwenda na kurudi Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.