HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR MHE. MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KATIKA UZINDUZI WA KONGAMANO LA MUUNGANO NA MCHAKATO WA MABADILIKO YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA MWAKA 1977 KATIKA UKUMBI WA EACROTANAL, TAREHE 13 JUNI, 201
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar na watendaji mliohudhuria
Mheshimiwa Mwakilishi wa Ford Foundation Ofisi ya Afrika Mashariki
Waheshimiwa Viongozi wa Taasisi mbali mbali za Serikali na za Kiraia
Waheshimiwa Wageni wote waalikwa nyote Mabibi na Mabwana
ASSALAM ALEYKUM.
Awali ya yote hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenye wingi wa rehma kwa kutujaalia afya njema na kutukutanisha hapa, kwa ajili ya kujadiliana masuala muhimu ya Muungano wa Tanzania na Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
Aidha, natoa shukurani zangu za dhati kwa Asasi mbili za Kiraia yaani Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar na Ford Foundation Ofisi ya Mashariki mwa Afrika yenye Afisi zake mjini Nairobi, Kenya.
Nakupongezeni kwa mashirikiano yenu na ubunifu wenu wa kutayarisha mkusanyiko huu ambao umekuja katika wakati muafaka.
Vile vile sina budi kutoa shukurani zangu nyingi kwenu waandalizi wa Kongamano hili, kwa uamuzi wenu wa kunialika mimi kuja kujumuika nanyi. Kwangu mimi binafsi hii naona ni heshima kubwa mliyonipa na ninaithamini sana, nasema Ahsanteni.
Niruhusuni nichukua nafasi hii kuipongeza Afisi ya Ford Foundation katika Afrika Mashariki kutimiza miaka 50 tokea ilipoanza shughuli zake katika Afrika Mashariki mwaka 1962. Aidha, naiomba Ford Foundation yenye Makao Makuu yake huku New York iendelee kushirikiana na Asasi za kiraia hapa Zanzibar katika sekta mbali mbali.
Tunaishukuru pia Ford Foundation kwa kuisaidia Zanzibar katika maeneo tofauti kwa mfano Tamasha la Filamu; Idara ya Nyaraka, Makumbusho na Mambo ya Kale; Tamasha la Nchi za Jahazi; Chama cha Waandishi wa Habari Zanzibar; na Jumuiya ya Asasi Zisizo za Kiserikali Zanzibar.
Huu ni msaada mzito na wenye maana kubwa kwa nchi yetu. Sisi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunatambua na kuthamini mchango huu mkubwa kwa nchi yetu. Kinachodhihirika wazi hapa ni kwamba, malengo ya Asasi mbili hizi yanafanana au tuseme yanashabihiana, na ndio sababu mukaweza kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kafanikisha maandalizi ya Kongamano hili ambalo tunategemea litakuwan na faida na maslahi kwa nchi yetu na wananchi wake.
Nashawishika kusema hayo kwa kuzingatia ule msemo wa Waingereza usemao “Ndege wa aina moja huruka pamoja” yaani “Birds of the same feather fly together”. Kwa kifupi Madhumuni ya Asasi hizi ni kusaidia wanyonge, ili nao wapate haki na kudumisha heshima ya binadamu na Utawala wa Sheria.
Waheshimiwa Waalikwa wa KongamanoMada ya Kongamano hili yaani Muungano na Mchakato wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ni mada nyeti ambayo inamgusa kila Mtanzania. Kutokana na ukweli huo, ni matarajio yangu wajumbe wa Kongamano mtatumia ujuzi, uwezo na uzoefu wenu mkubwa kufanya mjadala ulio hai, usiokuwa na jazba, ambao hatimaye utazaa mawazo na fikra zitakazosaidia kupata Katiba iliyo nzuri inayojali maslahi ya Watanzania wote, iwe wa Tanzania Bara au wa Zanzibar.
Mjadala juu ya Muungano wa Tanzania ni mada kongwe, ambayo wasomi, wanasiasa, wananchi mbali mbali na hata wageni wamekuwa wakiijadili mara kwa mara kwa mapana, na kwa mitazamo tafauti tokea Muungano huo ulipoasisiwa mwaka 1964. Wapo miongoni mwao wanao usifu Muungano wetu kuwa ni Muungano mzuri na wa mfano kutokana na kudumu kwake. Hao wana sababu zao, kati ya hizo ni nchi kadhaa za Afrika zilijaribu kuungana lakini baada ya muda mfupi, nchi hizo zilijikuta katika mizozo na migogoro hatimaye zilitengana.
Baadhi ya nchi hizo ni pamoja na Ghana na Guinea zilizoungana mwaka 1958, Muungano wa Senegal na Gambia (Senegambia Confederation) wa Mwaka 1982 hadi 1989, Muungano wa majaribio wa Libya, Tunisia, Mauritania, Morocco na Algeria (Muungano wa Maghreb) wa mwaka 1956, Muungano wa Misri na Syria wa Mwaka 1958 (United Arab Republic) ambao ulivunjika baada ya miaka mitatu hapo mwaka 1961.
Aidha, watu wengi duniani wakiwemo wasomi mashuhuri, wanafalsafa, wanasiasa waliobobea na wachambuzi wa mambo wanajiuliza kuna siri gani hata Muungano wa Tanzania uliotokana na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika umedumu kwa muda wa miaka 48 na bado unaendelea.
Maswali mengine yanayouulizwa ni pamoja na kwamba, Jee Muungano huu ni wa watu wawili? Yaani waliouasisi Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume au Muungano huu ni wa watu wote?
Jee, Muungano huu ulikusudiwa uwe wa muda, kutokana na mazingira yaliyokuwepo wakati huo? Jee, Muungano huo unakidhi sheria za Kimataifa? Jee, Muungano huu ni wa kisiasa? Kwanini hakuna manung’uniko mengi kuhusu Muungano huu?
Mimi binafsi naamini sina jukumu la kujibu maswali yote hayo. Bali Watanzania wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano watapata nafasi ya kutoa mawazo yao mbele ya Tume iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa madhumuni ya kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Lakini angalau kuhusu hili swali la mwisho linalouliza kwamba kwanini kuna manung’uniko ndani ya Muungano? Hili liko wazi. Ni kweli kuwa kumekuwa na manung’uniko mengi na ya muda mrefu juu ya Muungano wetu.Tume mbali mbali ziliundwa kuangalia malalamiko au kama wengine wanavyoziita kero za Muungano, na zote zimethibitisha kuwepo kwa manung’uniko hayo, na hata kupendekeza hatua za kuchukuliwa kutokana na wakati husika.
Katika uhai wa Muungano huu, wengine wanasema wanabanwa, wanafinywa, wanaumizwa, wanabebwa, wanajitutumua na wanajitanua.Miongoni mwa Tume zilizoundwa ni pamoja na Tume ya Mheshimiwa William Shellukindo juu ya Changamoto za Muungano, Tume ya Jaji Francis Nyalali kuhusu mfumo wa Vyama vya siasa nchini na Kamati ya Jaji Robert Kisanga kuhusu White Paper iliyotolewa na Serikali.Kwa upande wa Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo iliwahi kuunda Kamati kadhaa kushughulikia kasoro zilizopo katika Muungano.
Kwa mfano, Kamati ya Mheshimiwa Amina Salum Ali mwaka 1992, Kamati ya Baraza la Mapinduzi kuhusu Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 1990 na Kamati kuhusu Marekbisho ya Sera ya Mambo ya Nje mwaka 1999.
Pamoja na Kamati zote hizo na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati hizo, bado kero za Muungano hazikumalizika. Na badala yake mara nyingi matokeo ya Tume yalikuwa chachu ya kuibua mijadala mipya juu ya kero za Muungano.
Waheshimiwa Waalikwa wa Kongamano Katika zama hizi tulizonazo, ambapo misingi ya demokrasia inapewa nafasi ya kipekee, hatuna budi kuendelea kuyajadili mambo kama haya ambayo yanagusa maisha na maslahi ya wananchi walio wengi kwa uwazi mkubwa.
Vyama vya siasa na baadhi ya jumuiya za Kiraia nchini zimekuwa mstari wa mbele katika kujadili suala la Muungano kwa dhamira moja tu ya kuwa na mfumo au utaratibu utakaoleta haki na kuondoa malalamiko yaliyopo.
Wapo wanaosema dawa ya matatizo haya ya Muungano ni kuwa na serikali moja tu, wapo wanaosema tuendelee kuwa na serikali mbili huku tukitatua kero zinazojitokeza, wapo wanaosema tuwe na serikali tatu. Na nyote ni mashahidi, wapo wanaokuja na mawazo na fikra kwamba Muungano huu tuuvunje kabisa. Au kama wengine wanavyosema ‘tugawane mbao’.
Aidha, hivi sasa kumekuwa na mtazamo mpya ambao ni kufanya marekebisho ya Muundo wa Muungano, ili kuwe na Serikali mbili ambazo ni Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye uhuru na mamlaka kamili ya kujiamulia mambo yake, na Serikali ya Tanganyika yenye uhuru na mamlaka kamili ya kujiamulia mambo yake. Kisha Muungano utakaoanzishwa kwa njia ya mkataba, kwa mambo ambayo nchi mbili hizi watakayo kubaliana.
Wenye mawazo ya mfumo huu wanaamini kuwa huo ndio mwarubaini wa matatizo ya Muungano yanayodumu muda mrefu na ambayo yanaendelea kujitokeza. Mfumo wa Muungano wa mkataba si jambo geni na umekuwa maarufu sana hivi sasa Duniani. Hata Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya (European Union) ni mfumo wa aina hii ya Muungano.
Chini ya utaratibu huu kila serikali inakuwa na mamlaka kamili, lakini katika baadhi ya mambo wanayokubaliana yawe ya pamoja nchi husika zinafungana mikataba ya kuyaendesha na kuyasimamia.
Naamini kwa Wazanzibari lililo muhimu zaidi ni Muungano, na si haki kuwazuia Wazanzibari wasitoe maoni yao juu ya Muungano. Na kwa maana hiyo kwetu lililo muhimu zaidi ni hili la Muungano.
Waheshimiwa Waalikwa wenzanguMimi ni mmoja miongoni mwa viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Siasa cha CUF. Lakini pia mimi ni Mzanzibari na Mtanzania.
Kwa hiyo nitakuwa na haki ya kutoa maoni yangu wakati ukifika. Tuombe Mwenyezi Mungu atujaalie uhai.Hata hivyo, nachukua nafasi hii kuendelea kuwahimiza na kuwashauri Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kuzisoma Hati mbali mbali za Muungano, Katiba za Tanganyika, Katiba za Tanzania na Katiba za Zanzibar na maandiko mbali mbali ya wasomi katika vitabu au magazeti. Wakati utakapofika Tume ya Katiba itakapokuja wananchi waweze kuchangia huku wakiwa wanajua kwa undani Muungano wetu, ikiwemo faida na kasoro zake na waseme bila ya woga wanachokitaka.
Hii ni fursa adhimu ambayo wengi wamekuwa wakiililia kwa siku nyingi juu ya haja ya Watanzania kupata fursa ya kutoa maoni yetu, juu ya masuala yote yanayohusiana na Muungano.Wananchi wawe huru kutoa maoni yao kwa uwazi na pawepo na uvumilivu.
Hata kama mtu hakubaliani na maoni, hoja zinazotolewa na mwengine, inabidi asikilize kwa uvumilivu. Naye akipata fursa aseme yake kwa uwazi pia.
Waheshimiwa Waalikwa wenzanguNaomba kutoka nasaha zangu kwamba katika mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi juu ya mabadiliko ya katiba, ni vizuri sote tukatumia busara ya hali ya juu, hekima na uvumilivu, ili mchakato uende kwa salama.
Tukumbuke kuwa vurugu na misuguano ya aina yoyote haina faida na isipewe nafasi katika kutoa maoni yetu kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba. Na mwisho wa yote hayo, ni lazima tukubaliane kwamba maoni ya wengi yaheshimiwe baada ya wale wachache kupewa haki yao ya kusikilizwa kwa kikamilifu.Naomba kuchukua nafasi hii kuwatoa wasi wasi wananchi na hasa Wazanzibari.
Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi wametokana na Wazanzibari wenyewe. Viongozi hao ni Wazanzibari kindaki ndaki, wenye kujawa na kiwango kikubwa cha uzalendo. Wanaipenda Zanzibar kama Mzanzibari mwengine yoyote yule.
Viongozi wapo kulinda maslahi ya Zanzibar na watu wake, kama vile viongozi wa Tanganyika walipo kulinda maslahi ya wananchi wenzao wa Tanganyika. Kwamwe viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hawata wasaliti wananchi wa Zanzibar. Tutaheshimu na kutetea maoni yenu wananchi kama mlivyo yatoa kwa Tume ya Jaji Warioba.
Muhimu jitokezeni kwa wingi mtoe maoni yenu. Maoni ya wengi naamini yataheshimiwa.
Naomba nitahadharishe watu wasijefanya kosa la kuto kwenda kutoa maoni yao. Kama mtu hakwenda anaweza kuja kujilaumu, pale ambapo maoni ambayo yeye hayaungi mkono yakaja kuwa ndio maoni ya wengi, kwa sabababu tu yeye na wenziwe wenye maoni kama yake hawakujitokeza kutoa maoni yao.
Baada ya kusema hayo machache nachukua nafasi hii kukushukuruni nyote kwa kunisikiliza kwa makini na sasa natamka kwamba kongamano la Muungano na Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba limefunguliwa rasmi.
Ahsanteni.
Hotuba ni nzuru na itawaamsha wale waliolala au wasiofahamu undani wake lakini kwa ufupi wananchi twendeni tukatoe maoni yeatu kwamba muungano sasa basi tugawane nbao.
ReplyDelete