Na Othman Khamis, OMPR
CHUO Kikuu cha Brown kilichopo mjini Boston
nchini Marekani, chini ya taasisi inayoshughulikia taaluma ya teknolojia ya
afya (MED International), kinakusudia kuipatia Zanzibar mashine ya uchunguzi wa
vinasaba (DNA).
Mashine hiyo inatarajiwa kuwasili nchini
muda wowote kuanzia mwezi Julai mwaka huu, ambapo kupatikana kwake kunatokana
na ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi,
aliyoifanya mwezi Oktoba mwaka jana.
Mkurugenzi wa MED International, Jayson
Marwaha, alithibitisha kuwa taasisi yake itaipatia mashine ya DNA, wakati
alipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali
Iddi huko ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Katika zaiara hiyo, Jayson alifuatana na
Mkurugenzi mwenza wa Han Sheng Chia, walimueleza Balozi Seif, sambamba na msaada huo wamekuja Zanzibar
kufanya utafiti wa afya katika hospitali tofauti za serikali za Unguja na
Pemba.
“Lengo letu kufanya utafiti wa afya hapa
Zanzibar, lakini pia tutaangalia maeneo na vifaa vinavyohitajika na tutakaporejea
kwenye taasisi yetu tuweze kuchukua kwa nia ya kuimarisha ustawi wa Jamii hasa
ile ya kawaida”, alisema Mkurugenzi huyo.
Jayson, alieleza kwamba katika kuona taaluma
ya kiuhandisi ndani ya sekta ya afya inakuwa kiteknolojia taasisi yake
inatarajia pia kuleta mabingwa wa fani hiyo mnamo mwezi wa Agosti mwaka huu.
Katika mazungumzo yao nchini Marekani mwaka
jana, Jayson aliwahi kumuahidi Balozi Seif kwamba taasisi yake itaandaa
taratibu kwa wataalamu wake kufanya kazi za kujitolea hapa Zanzibar.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza taasisi hiyo inayoshughulikia taaluma ya
teknolojia ya afya kwa uamuzi wake wa kusaidia huduma za afya hapa Zanzibar.
Balozi Seif, alielezea kufarajika kwake na
ujio wa uongozi wa juu wa taasisi hiyo ambao umeonyesha uungwana katika
kutimiza ahadi zake ilizozitowa mwaka jana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza
ujumbe huo kwamba serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuimarisha zaidi
huduma za afya katika hospitali zake zote Unguja na Pemba.
Mapema Naibu waziri wa Afya Zanzibar Dk.
Sira Ubwa Mwamboya, alisema ujumbe huo umekuja wakati muwafaka kwa vile bado
eneo la fani ya sayansi katika chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni inahitajika.
Wakati huo huo, Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alikabidhi msaada wa gari moja kwa ajili ya
matumizi ya shughuli za Jumuiya ya Fiy Sabilillah Markaz ya Fuoni.
Balozi Seif, alisema yeye binafsi, familia
yake na wafadhili wameamua kutoa msaada huo kutokana na mchango mkubwa
unaotolewa na Jumuiya hiyo ndani katika kueneza Daawa kwa jamii.
Mapema katibu wa Jumuiya ya Fiy Sabilillah
Markaz ya Fuoni, Sheikh Mwalimu Hafidh Jabu, aliuomba uongozi wa serikali kuwa
karibu zaidi na Jumuiya hiyo kwa lengo la kufanikisha majukumu waliyojipangia.
No comments:
Post a Comment