Na Salum Vuai, Maelezo
VIONGOZI na wanachama wa klabu kongwe ya soka hapa Zanzibar timu ya Miembeni SC, wamekutana klabuni kwao juzi kutathmini hali ya timu hiyo na kutafuta namna ya kuirejeshea hadhi yake.
Khamis Mussa anayeshikilia nafasi ya ukatibu mkuu wa timu hiyo, ameliambia gazeti hili baada ya mkutano huo kuwa, ajenda kuu iliyotawala ilikuwa suala la kuifanyia marekebisho katiba ya klabu ili kuruhusu uchaguzi wa kutafuta viongozi wapya.
Alifahamisha kuwa, uongozi wa sasa si halali kwani umekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 30, huku kukiwa hakuna uchaguzi wowote uliofanyika.
Mussa alitoa mfano kwa kusema kuwa, yeye akiwa katibu, aliomba ruhusa kwenda masomoni zaidi ya miaka kumi iliyopita, lakini alirudi na kuendelea na wadhifa wake hadi sasa, huku timu hiyo ikibadili mikono ya ufadhili kila mara na kusababisha mivutano isiyokwisha.
"Kwa miaka mingi sasa, timu imekuwa na viongozi haohao, Mwenyekiti Haji Ali, mimi katibu na wengine, pengine hili ndilo linaloibua matatizo na malumbano na hivyo kukosa maendeleo", alifafanua.
Ili kulipatia ufumbuzi suala hilo, Mussa alisema mkutano wao uliamua kuteua wanachama kadhaa kwenda kwa Mrajis wa Vyama vya Michezo Zanzibar, ili kuangalia mapungufu yaliyomo katika katiba, na kutafuta muongozo wa kuifanyia marekebisho na baadae kufungua milango ya kufanyika kwa uchaguzi ili kupata viongozi halali.
No comments:
Post a Comment