Habari za Punde

Taifa Stars yawapa raha Watanzania . Magoli ya Kapombe, Nyoni yailewesha Gambia

DAR ES SALAAM
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, jana iliutumia vyema uwanja wa nyumbani wa Taifa, kwa kuichapa Gambia mabao 2-1 katika mechi ya kusaka tiketi ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 zitakazochezwa nchini Brazil.

Stars iliyoshuka dimbani ikikumbuka kipigo cha magoli 2-0 mbele ya Ivory Voast jijini Abidjan siku 12 zilizopita, iliweza kuwabana wachezaji wa Gambia ingawa nao walikianza kipindi cha kwanza kwa kasi na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga.

Katika pambano hilo lililochezeshwa na waamuzi kutoka Zimbabwe, The Scorpions iliwatumia washambuliaji wake Musa Camara, Abdou Jammeh, Lamin Basmen, Ousman Koli na wsengine kuichanganya ngome ya Stars iliyokuwa ikipangwa vyema na mlinda mlango Juma Kaseja.

Wagambia walikuwa wa kwanza kuzifumania nyavu za Stars kwa bao la dakika ya nane lililofungwa na Mamadou Cesay.

Bao hilo liliizindua Stars na kuanza kuliandama lango la wapinzani wao kwa mashambulizi ya mfululizo, ingawa ilikumbana na ukuta mgumu wa timu hiyo ambao ulimudu kulinda bao lake hadi wakati wa mapumziko.

Hata hivyo, Stars ilicheza ovyo kidogo, lakini kuingia kwa Haruna Moshi ‘Boban’ aliyechukua nafasi John Bocco ‘Adebayor’ kipindi cha pili, kuliifanya Tanzania ipate uhai na kulitia misukosuko lango la Gambia hatimaye kupata mabao hayo mawili.

Mara kadhaa washambuliaji wa timu hiyo Haruna Moshi, Mrisho Ngassa, Shomari Kapombe na Mbwana Samatta, walijaribu kuingia ndani ya nyavu za Gambia, bila mafanikio.

Taifa Stars ilikianza kipindi cha pili kwa kasi na dhamira ya kubadilisha matokeo, ambapo wachezaji wake walihaha kila sehemu kusaka mabao na kuipa wakati mgumu safu ya ulinzi ya Gambia.

Jitihada za Stars, ziliiwezesha kusawazisha bao katika dakika ya 61 kupitia kwa mchezaji wake Shomari Kapombe, na kuamsha nderemo katika majukwaa ya mashabiki waliokuwa na shauku ya kuziona nyavu za Wagambia zikichanwa.

Erasto Nyoni, aliwapa ahueni Watanzania alipofanikiwa kuandika bao la pili na la ushindi katika dakika 84 kwa mkwaju wa penelti.

Kwa matokeo hayo, Taifa Stars inashika nafasi ya pili katika kundi C, ikifikisha pointi tatu nyuma ya vinara Ivory Coast wenye pointi nne, huku Morocco ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi mbili, na Gambia ina pointi moja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.