Habari za Punde

Muhtasari Bajeti Mpya. Serikali Kutumia 648.9 bn/ Uchumi Kukua kwa 7.5%. .Vipaumbele Kilimo, Afya, Elimu

Na Mwantanga Ame
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo Omar Yussuf Mzee, amesema kuwa bajeti ijayo itaangalia zaidi uimarishaji wa miundo mbinu, nishati, kilimo pamoja na huduma za jamii.

Waziri huyo alieleza hayo jana ofisini kwake mjini Zanzibar alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoa muhtasari wa bajeti mpya ya mwaka 2012- 2013, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 648.9 zinatarajiwa kutumika.

Alisema katika bajeti hiyo suala la miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara na uwanja wa ndege vitapewa kipaumbele kwani ndio msingi mkuu wa uchumi wa Zanzibar.

Aidha alisema suala ni nishati ya umeme nalo litapewa umuhimu, kilimo cha umwagiliaji maji ambapo msingi wake kimelenga kuongeza uzalishaji wa chakula.

Akizungumzia suala la afya kama kipaumbele chengine katika bajeti ijayo, waziri huyo alisema serikali inakusudia kuiandalia mazingira bora kwa kuanzisha mpango wa kununua dawa na vifaa vyenye kuhitajika katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Aidha waziri huyo alibainisha kuwa eneo jengine ambalo serikali italipa umuhimu ni suali la ajira kwa vijana ambapo mkakati utaandaliwa kwa kushirikiana na vyuo viliopo nchini kwa kuhakikisha wanachukua wanafunzi ambao wataendana na soko la ajira hapa nchini.

Waziri huyo alifahamisha kuwa serikali katika mwaka ujao itaendelea na mipango yake ya kuwahudumia wazee sambamba na kuwasaidia watu wenye ulemavu.

Akizungumzia sekta ya elimu, alisema itaendelea kuimarishwa kwa kuhakikisha vifaa vya masomo ya sayansi vinapatikana mpango ambao utaenda sambamba na kukuza watoto wa kike kupenda masomo ya hesabati.

Akizungumzia ukusanyaji wa mapato na uchumi kwa uiumla, waziri Mzee alisema ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka ujao wa fedha utafikia shilingi bilioni 294.1 ambazo ni sawa na asilimia 21.3.

Alisema mchango wa washirika wa maendeleo kwa mwaka ujao wa fedha serikali itapokea shilingi bilioni 333.2 na matumizi ya serikali yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 307.8 ambapo kati ya fedha hizo mishahara ya wafanyakazi wa serikali ni asilimia 47.4.

Alisema katika mwaka ujao wa uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kutoka asilimi 6.8 ya mwaka 2011, nakufikia asilimia 7.5 kwa mwaka 2012/2013, ambapo pia mfumko wa bei unatarajiwa kushuka kufikia asilimia 8.7 baada ya kuonesha viashiria vya mabadiliko ya kiuchumi duniani.

Upande wa pato la ndani la taifa waziri huyo, alisema hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu lilifikia asilimia 18.5 huku mchango wa washirika wa maendeleo ulifikia shilingi bilioni 371.3 ikiwemo ya misaada na mikopo.

Alisema licha ya uchumi wa Zanzibar kukua, lakini suala la mfumko wa bei limeongezeka kufikia asilimia 14.7 kutoka asilimia 6.1 ya mwaka 2010, ambapo hali hiyo ilitokana na hali ya mabadiliko ya kiuchumi duniani.

Alisema pato la mwananchi kwa bajeti iliopita nalo limekuwa kutoka shilingi 782,000 kwa mwaka, hadi kufikia shilingi 960,000 ambazo ni sawa na dola za kimarekani 615 kutoka dola 560 ya mwaka 2010.

Alisema kiwango hicho kimeifanya Zanzibar, kuyapita malengo ya milenia ambapo nchi zote duniani zinatakiwa ifikapo 2015, pato la mwananchi kufikia shilingi 884,000 kwa mwaka.

Akizungumzia suala la utawala bora, alisema suala hilo litaimarishwa
kwani ni sehemu ya msingi itayoweza kuwepo matumizi bora ya fedha za serikali kwa kufuata sheria na kanuni za fedha pamoja na kuweka mazingira bora katika taasisi za Mahakama na Vyuo vya Mafunzo.

Akizungumzia juu ya bajeti iliopita kwa mwaka wa fedha 2011/2012 Waziri huyo alisema imepata mafanikio makubwa kwa kuweza kuyafikia maeneo matatu makuu ikiwemo ya utekelezaji wa mpango wa taifa wa dira 2020, Utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Mpango wa Kupunguza Umasikini MKUZA.

Alisema kwa mwaka uliopita serikali ilipanga kutumia shilingi bilioni 321.5, lakini walilazimika kutumia shilingi bilioni 377 ikiwa ni sawa na asilimia 100.3 jambo ambalo limetokana na kupandisha viwango vya mishahara kwa watumishi wa umma.
 
 
 
Alisema bajeti hiyo ilipata changamoto mbali mbali ambazo zilionekana kwenda sambamba na zile za dunia, lakini hazikuweza kuifanya Zanzibar kuingia katika msukosuko wa kibajeti ikilinganishwa na mataifa mengine.

Alisema uchumi wa dunia kwa mwaka 2011 haukuwa katika hali nzuri ikilinganishwa na mwaka 2010 ambapo kwa mwaka 2010 ulifikia asilimia 5.3 na mwaka 2011 ulishuka na kufikia asilimia 3.9.

Kwa nchi zilizoendelea Waziri huyo alisema uchumi wake ulifikia asilimia 3.2 kwa mwaka 2010 na mwaka 2011 ulifikia 1.6 huku nchi zinazoendelea uchumi wake ulifikia asilimia 5.9 na Nchi ziliomo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki zilifikia 4.6 hadi mwaka 2011.

Kuhusu mfumko wa bei alisema katika nchi zilizoendelea ulipanda kwa mwaka 2010 ulikuwa ni asilimia 1.6 na 2011 ulifikia asilimia 2.7 na nchi zinazoendelea kwa mwaka 2010 ulikuwa asilimia 6.1 na mwaka 2011 ulifikia asilimia 7.2 huku kwa nchi za Afrika Mashariki ulitoka asilimia 6.1 kwa mwaka 2010 na kufikia asilimia 9.6 kwa mwaka 2011.

Alisema jambo la msingi litalohitajika kuona linafanywa kwa hivi sasa ni kuhakikisha kila mwananchi anadumisha amani ili kuiwezesha bajeti ijayo kuwa ni yenye mafanikio.

Aidha, Waziri huyo alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanashiriki vyema katika zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Waziri huyo pia aliwataka wananchi kuona wanajiamdaa kushiriki vyema katika zoezi la kutoa maoni yao katika mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.