Na Hafsa Golo
WAZIRI wa Elimu Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamuhuna amesema milango ipo wazi kwa kuacha kazi kwa walimu ambao hawapo tayari kutekeleza majukumu yao ya kazi pamoja na kuifuata sera ya elimu.
Waziri huyo alieleza hayo alipokuwa akizungumza na Walimu Wakuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja katika ukumbi wa Chuo cha Elimu ya Amali Mkokotoni huko Mkokotoni.
Waziri huyo alisema kuwa kama wapo walimu ambao hawataki kutekeleza majukumu yao kazi huku kiwango cha elimu kikiporomoka ni malngo upo wazi wa kuondoka.
"Kila mwalimu achague kusuka au kunyowa na atakae kiuka wajibu wake dawa ipo”, alisema waziri huyo.
Aidha aliwataka walimu wakuu kujenga tabia ya kuwafatilia walimu wanaofundisha wanafunzi na kuhakikikisha wanafuata sheria na taratibu na kile wanachokisomesha ili kuwajenga wanafunzi katika kujiamini kujibu masuali wakati wanapofanya mitihani yao ya taifa.
Waziri huyo aliwataka walimu hao kuondosha muhali katika kutekeleza wajibu wao katika utendaji wa kazi zao na wahakikishe wanafanyakazi kwa uadilifu ili kuondosha aibu iliojitokeza ya kufutiwa matokeo ya mitihani mwaka uliopita.
Akizungumzia athari zilizosababisha wanafunzi kufutiwa mitihani yao ni pamoja kukosekana kwa uadilifu kwa baadhi ya walimu kwani muda wa masomo walimu hao hujishughulisha na mambo yasiohusiana na majukumu yao ya kazi.
Alisema kuwa imefika wakati baadhi ya walimu wanajali zaidi masomo ya ziada kwa kisingizio cha kufata maslahi jambo ambalo limesababisha kuwafundisha wanafunzi kukopi mitihani yao.
"Tumewaandaa sisi watoto kujibu mitihani kwa njia za udanganyifu kwa kudhani hatutojulikana, leo aibu imetupata Wazanzibari, wanafunzi hawafundishwi taaluma wanafundishwa kukopi majibu yanafanana walimu wakuu simamieni hili lisije likatokezea",alisema.
Kwa upande wa mwalimu Mkuu wa skuli ya Fujoni, Mabrouk Is-haka Daima alisema kuwa si jambo la kawaida lililotokezea na hakuna mwalimu aliyelifurahia hivyo watahakikisha wanazidisha ari katika kusimamia majukumu yao.
Alisema maagizo aliyowapa waziri ni changamoto kwao katika utendaji wao na kuongeza juhudi katika usimamizi wa kazi zao za kila siku.
No comments:
Post a Comment