Habari za Punde

Utafiti: Tiba Asili za Macho Zasababisha Upofu


Na Fatma Kassim, MAELEZO
WIZARA ya Afya imesema utafiti uliofanywa mwaka 2007, umebainisha kuwa jamii kwa kiasi kikubwa inatumia dawa ya asili katika kutibu maradhi ya macho jambo ambalo linaweza kusabisha upotevu wa nuru na upofu.

Kaimu Mratibu wa Kitengo cha Macho, Issa Muhsin Burhan aliyasema hayo katika mafunzo ya msingi ya huduma ya macho kwa waganga wa jadi na tiba asili wa Mkoa wa Kusini na Kaskazini Unguja yaliyofanyika wizara ya Afya.

Alisema athari za dawa asili katika kutibu macho ni pamoja na kuficha dalili na ishara za maradhi hayo na kusababisha uambukizo mbaya katika jicho na kupelekea upofu.

Aidha alifahamisha kuwa baadhi ya waganga wanatumia tiba asili katika kutibu maradhi ya macho bila ya kujua athari zake na kuchelewesha tiba sahihi na hivyo kusababisha athari kubwa kwa watumiajia wa dawa hizo.

Alisema lengo la kuwapatia mafunzo hayo waganga, ni kuleta maelewano na kitengo cha macho na kujua utambuzi wa dalili na ishara za maradhi hayo pamoja na kupanga mikakati ya tiba ya ruifaa kwa wagonjwa wenye matatizo makubwa kwa kuwapeleka hospitali na sio kuwapa tiba asili.

Aliwataka waganga hao kusaidia jamii kwa kuepuka upofu usiowalazima kwa kuhimiza jamii kufanya uchunguzi wa macho mara wanapopata uambukizo na watoto wachanga wachunguzwe hospitalini na kuepuka kutiwa maziwa ya mama kwani yanasababisha madhara makubwa.

Nao washiriki wa mafunzo hayo, alisema awali walikuwa hawatambui madhara ya dawa asili kwa macho ambapo kutokana na mafunzo hayo kumewezesha utambuzi wa athari za dawa asili.

Walikuwa wakitumia dawa za asili kwa kuwapatia wagonjwa wenye matatizo ya macho lakini kutokana na mafunzo hayo waliyoyapata watahakikisha wanapopata mgonjwa wa macho wanamshauri afike hospitali mara moja kwa kuepuka athari zisitokee.

Mafunzo kama hayo yanatarajiwa kuwafikia waganga wote wa Unguja na Pemba ambapo kwa kuanzia yamefanyika kwa waganga wa Kusini na Kaskazini Uguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.