Habari za Punde

Wachina Wapeleka Huduma za Afya Fuoni


Na Salum Vuai, Maelezo
TIMU ya madaktari 21 kutoka Jamhuri ya Watu wa China, imeendelea na programu yake ya kutoa huduma za kiafya na tiba katika vituo mbalimbali Unguja na Pemba.

Kumi na mbili kati ya madaktari hao, wanaendelea na kazi hiyo hapa Unguja, na tisa wamepiga kambi katika hospitali ya Abdallah Mzee Mkoani

Katika muendelezo wa mpango huo, jana timu ya madaktari kumi wa maradhi mbalimbali, waliendesha kliniki katika kituo cha afya cha Fuoni Wilaya ya Magharibi Unguja, ambapo zaidi ya wananchi 160 walifika na kuchunguzwa afya zao na kupatiwa huduma.

Miongoni mwa huduma hizo, ni uchunguzi wa maradhi ya masikio, macho, meno, matatizo ya wanawake, homa za kawaida, mifupa na mengineyo.

Katika mpango huo, baadhi ya wananchi walioonekana na matatizo ya kiafya, walipewa dawa na ushauri, na wengine walielekezwa kufuata huduma zaidi hospitali kuu ya Mnazimmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari, kiongozi wa wataalamu hao Dk. Lu Jianlin, alisema mpango huo unaofadhiliwa na Jamhuri ya Watu wa China, unalenga kuwasaidia wananchi wa Zanzibar kuondokana na matatizo ya kiafya, ili taifa lao liwe na watu wenye siha na nguvu watakaoweza kuliletea maendeleo.

Alisema ni fahari kwa nchi yake kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha huduma za afya, na kwamba mpango wa kuleta madaktari wa kujitolea ulianza tangu miaka 47 iliyopita na kuleta mafanikio makubwa kwa wananchi wa hapa.

Alieleza kuwa, kila mwaka serikali ya nchi yake imekuwa ikitoa yuan bilioni moja (sawa na dola 160,000 za Kimarekani) kwa ajili ya kusaidia huduma za afya.

"Mpango huu ambao nchi yangu inasaidia, ni njia nzuri ya kuimarisha uhusiano wa kidugu uliodumu kwa muda mrefu kati ya nchi zetu mbili", alieleza Dk. Jianlin.

Daktari dhamana wa kituo cha afya Fuoni Abdulhalim Mohammed Ali, alisema uzoefu unaonesha kuwa matatizo makubwa yanayowakabili wananchi wa Fuoni na maeneo ya jirani, ni meno na macho, lakini akaishukuru timu ya madaktari wa Kichina kwa kuamua kupeleka huduma kituoni hapo.

Aidha, alisema katika siku za kawaida, maradhi ya mripuko yakiwemo matumbo ya kuharisha, yamekuwa yakiibuka sana, hali inayosababisha msongamano kubwa katika kituo hicho, kutokana na udogo wake.

Daktari huyo ameiomba serikali kufanya utaratibu wa kukitanua kitu hicho ambacho kwa sasa kimezungukwa na nyumba za makaazi na kusababisha usumbufu katika utoaji wa huduma hasa za kulaza wagonjwa.

Baadhi ya wananchi waliofuata huduma za madaktari wa Kichina kituoni hapo, walishukuru kwa mpango huo na kusema kuwa miongoni mwao wamekuwa wakisumbuka kwa muda mrefu kwa matatizo mbalimbali ya kiafya, na kueleza matumaini yao kuwa tiba walizopatiwa zitawasaidia kupona.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.