Na Mwandishi wetu, Moshi
MWANZILISHI wa mbio za marathoni za Mlima Kilimanjaro
Marie Frances kutoka Marekani, amemwagia sifa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa
ni kiongozi anayependa nchi yake na anayeona mbali.
Marie Frances ametoa sifa hizo mjini Moshi wakati Rais
Kikwete alipokuwa akikutana na viongozi wa Chama cha Riadha Tanzania (AT), kwa
ajili ya kupanga mikakati ya kufufua riadha nchini.
Frances ambaye aliwahi kukutana na Rais Kikwete wakati
wa ufunguzi wa jengo la Tanzania House katika jiji la Washington DC, amesema
kuwa ni nadra sana kuona kiongozi wa nchi akikutana na viongozi wa chama cha
mchezo wowote kuzungumzia maendeleo yake, na kusema hiyo ni miujiza hata katika
nchi kama Marekani.
Amemuelezea Rais Kikwete kama mtu wa haiba ya kipekee
mwenye akili na maono ya kuiendeleza Tanzania kufikia malengo ya Umoja wa
Mataifa ya Millenia.
“Nilimpenda sana nilipokutana naye jijini Washington. Ni
kiongozi mwenye haiba ya kipekee” alisema Frances ambaye aliombwa na Balozi wa
zamani wa Tanzania nchini Misri kuja kuanzisha mbio za marathon nchini Tanzania
mwaka 1990.
Marie Frances ambaye alikuwa mkuzaji (producer) wa Miss
Universe pamoja na vipindi vya televisheni huko Hollywood nchini Marekani,
alihamia Misri mwaka 1984 kufanya kazi ya ABC akiwa mwandishi wa bahari.
Akiwa nchini Mirsi, Marie Frances alianzisha mbio za
Pyramid Marathon pamoja na Miss Universe ambazo ziliitangaza sana nchi hiyo.
Ni wakati wa matamasha haya balozi wa Tanzania nchini
Misri wakati huo alipomwomba aje Tanzania kuanzisha mbio za marathon ili
kuitangaza Tanzania.
Frances alikuja Tanzania mwaka 1990 na kutaka kuanzisha
mbio za ‘Mt. Meru Marathon’ lakini alipofika tu mjini Moshi alivutiwa sana na
mlima Kilimanjaro na hivyo kuamua kuanzisha mbio za ‘Mt. Kilimanjaro Marathon’
mwaka 1991.
Mbio hizo hufanyika kila Jumapili ya mwisho ya mwezi wa
sita na zitatimiza miaka 22 tarehe 24 Juni mwaka huu.
No comments:
Post a Comment