Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk. Shein amteuwa Marina Joel Thomas

Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein,amemteua Marina Joel Thomas kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Taarifa ya Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee,kwa vyombo vya habari imesema uteuzi huo umeanza Juni 17 mwaka huu.

Rais amefanya uteuzi huo chini ya kifungu 66 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Katiba ya Zanzibar inampa uwezo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuteuwa watu kumi kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Walioteuliwa kupitia nafasi hizo na nyadhifa zao za sasa kwenye mabano ni Balozi Seif Ali Idd(Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar), Mohammed Aboud Mohammed(Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais) Omar Yussuf Mzee(Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo).

Wengine ni Zainab Omar( Waziri wa Ustawi wa Jamii,Maendeleo Vijana Wanawake na Watoto), Ali Mzee Ali, Sira Mwamboya (Naibu Waziri wa Afya) Juma Duni Haji (Waziri wa Afya), Fatma Abdulhabib Ferej(Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais) Ramadhan Abdallah Shabaan( Waziri wa Ardhi, Maji na Maendeleo ya Makaazi) na Marina Joel Thomas.

Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinatarajiwa kuendelea kesho kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuanza kujadili bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyowasilishwa Jumatano wiki hii.

Katika bajeti yake SMZ inatarajia kutumia jumla ya TZS 648.9 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2012/13, ikiwa ni ongezeko la asilimia 38.2 kutoka shilingi 469.4 bilioni zinazotarajiwa kutumika hadi kufikia mwisho wa Juni mwaka huu.

Serikali pia inatarajia kuanza mwaka wa fedha ikiwa na bakaa ya shilingi 5.9 bilioni. Katika hotuba yake Waziri nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Fedha,Uchumi na Mipango ya Maendeleo,Omar Yussuf Mzee alisema kwa kuzingatia uwezo wa sasa wa Serikali katika mapato yake kutokana na vyanzo vya ndani, yanatarajia kufikia jumla ya shilingi 280.7 bilioni na hivyo kufanya jumla ya mapato hayo kufikia shilingi 286.6 bilioni.

Waziri huyo aliwaambiwa Wajumbe wa Baraza kwamba Fedha hizo ni mjumuisho wa mapato ya Kodi na yasiyo ya kodi, ambapo Kiasi hicho cha mapato cha shilingi 286.6 bilioni kitaacha nakisi katika Bajeti ya shilingi 362.3 bilioni.

6 comments:

  1. Kaka, jina pekee halitoshi, tunaomba data za ziada kama vile kabla ya uteuzi huu Mh. Marina alikua nani.

    Hata hivyo, nampongeza mh. Rais kwa kuzingatia uwakilishi wa jamii mbalimbali za kizanzibari bila kujali rangi, dini, kabila au jinsia.

    Najua jamaa zangu (uwamsho) itawauma sana hii! lkn itabidi wasubiri mpaka chama chao kiingie madarakani ndio wafanye hivyo wanavyotaka!

    ReplyDelete
    Replies
    1. Kwani nani aliesema kuwa Marina ni mkristo? Mbona unarukia tu. Kwanini liwaume UAMSHO hili, kwani watu wenye asili ya bara hawajawahi kuwa wawakilishi?(Mwakanjuki, Kisasi si walikuwa wakristo pia na wenye asili ya Tanganyika?)

      Delete
  2. @Adhubany, Huku Mashariki ya mbali Marina ni jina la kiislaam, na yapo mengi tu. Hata hivyo jina si ishu wadau. Wapo pia wanaoitwa John na wakawa waislaam, na wapo akina Omari ambao ni wakiristo. Mifano ipo mingi. Namkumbuka Prof. Omari yule aliyekuwapo UDSM miaka mingi, lakini alikuwa Padri hasa. Kwa hiyo musiwahukumu watu kwa kutumia majina yao.

    Ama kuhusu uamsho unawasingizia au unachuki binafsi nao. Hebu ingia Mzalendo.net usikilize hizo video zilizowekwa labda utajuwa msimamo wao kuliko kurusha makombora tu.

    ReplyDelete
  3. Sisi hatujali jina wala dini Zanzibar, Wakiristo tunao karne na karne na tumekuwa na kucheza nao; tunachojali ni Uzalendo wa mtu kwa nchi yake, je amekubali kuwa Zanzibar ni nchi yake na yuko tayari kuitumikia kwa moyo mmoja ama ndio hao tunaoetewa kuleta fujo. By the way siku hizi ukitetea haki ya nchi yako ya Zanzibar, basi wewe una msimamo wa uamsho!?

    ReplyDelete
  4. Mimi sikurupuki! UWAMSHO ni watu wangu nawajua vizuri na kila ijumaa tukirudi kwenye dua tunabishana kutokana najazba zao!

    Acheni hoja za kitoto! Ukikuta omari mkristo ujue murtadi huyo! na huku kwetu ukikuta Marina muislamu ujue 'convert' huyo!

    Ama kughusu mzalendo.net, mimi mdau pale na najua uwezo wa watu wangu na namna wanavyofikiri.

    Huwezi kutetea watu wasio jitambua! mimi nimewatete mwisho nimechoka saivi ukiona mwazo mbadala ujue mmoja nimi, mwengine 'Jemshid' mwengine 'kafiri orijino'

    Hebu leo soma mzalendo, kuhusu huo uteuzi wa MARINA ujue mimi sikurupuki!

    ReplyDelete
  5. Kuna mmoja ameuliza Swali la huyo bibi aliyetuuliwa kuwa atakubali kuitumikia nchi yake au yupo tayari kuitumikia nchi yake.Huyo Marina tayari anaitumikia nchi yake amezaliwa hapo Unjuja na anafanya kazi hapo Unguja muda mwingi tu.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.