Dar es Salaam
KLABU ya soka ya Simba SC, imeeleza kusikitishwa kwake na kitendo cha watani wao Yanga, kuvunja taratibu za usajili kwa kumrubuni mchezaji wake Kelvin Patric Yondani kwa kufanya kiinimacho ili aonekane amesaini kuichezea klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Jangwani na Twiga jijini Dar es Salaam.
Simba imedai kuwa, kitendo hicho cha Yanga kilimuonesha mchezaji huyo akiandikishwa makaratasi kwa ushahidi wa picha, na baadae kuripotiwa na vyombo vya habari kwamba alikuwa akisaini mkataba wa kuichezea timu hiyo ya Yanga.
Taarifa ya Mwenyekiti wa Simba Ismal Aden Rage, kwa waandishi wa habari jana, ilisema klabu hiyo ilipata mashaka baada ya kuona mtu aliyeonekana katika picha hiyo pamoja na Yondani, ni mjumbe wa Yanga aliyejiuzulu, Seif Ahmed.
Hata hivyo, alifahamisha kuwa, shaka kwamba ni Yanga iliyofanya utaratibu huo, iliondoka pale tovuti ya Yanga ilipotangaza kupitia tovuti yake kuwa imemsajili mchezaji huyo wa Simba, huku mbele yake katika picha hiyo kukionekana fedha, jambo alilosema linaonesha mazingira ya kurubuniwa.
"Kwa utaratibu wa kifedha, hasa pesa nyingi kiasi hicho, malipo yake yanapaswa kupitia benki", alieleza Rage..
"Mbali na hayo, picha inamuonesha Kelvin akiwa katika jezi ya mazoezi ya timu ya Taifa na yenye logo ya Kilimanjaro, na kumbukumbu zinaonesha mkataba kati ya TBL na TFF tarehe 9 Mei, 2012, kwa haraka haraka tukio hilo limefanyika katika kipindi chini ya mwezi mmoja ingawa taarifa za ushahidi zinaonesha limetokea jana (juzi) tarehe 6 Juni, 2012", alizidi kufafanua Rage.
Katika maelezo yake, Rage alisema Simba haipendi kuamini kwamba tukio hilo liliihusu klabu ya Yanga, kwani Seif Ahmed alikwishajiuzulu kutoka kwenye kamati ya timu hiyo na pia Yanga ni klabu kongwe na inayojua taratibu zote za usajili.
Taarifa ya Mwenyekiti huyo ilibainisha kuwa, klabu yake imeshawasiliana na jopo lake la mawakili, na inajiandaa kuishtaki Yanga katika mamlaka inayohusika na kudai adhabu ya kutopitisha majina yote ya usajili ya Yanga kwa mwaka 2012/2013 na miaka mingine miwili ijayo, na kusema Simba iko tayari kufuatilia suala hilo hadi katika mahakama ya mpira ya FIFA.
Rage alihitimisha kwa kusema, Kelvin Yondani ni mchezaji halali wa Simba ambaye mkataba wake unamalizika Mei 31, 2014 baada ya kuongezwa Disemba 23, mwaka jana.
No comments:
Post a Comment