ERBIL, Kurdistan
TIMU ya Taifa ya Zanzibar, 'Zanzibar Heroes, imefanikiwa kutnga nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia kwa nchi zisizokuwa wanachama wa Shirikisho la Kimataifa (Fifa), VIVA World Cup'.
Hatua hiyo inafuatia Heroes kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tamil Eelam katika mchezo wa pili na wa mwisho kwenye kundi B, uliochezwa katika dimba la Erbil.
Mabao ya Zanzibar Heroes katika mtanange huo, yalifungwa na Mcha Khamis katika dakika ya 22, Amir Hamad dakika ya 62, na Awadh Juma aliyezifumania nyavu mnamo dakika ya 90 ya mchezo.
Kwa matokeo hayo, Zanzibar inatarajiwa kupambana na Cyprus ya Kaskazini katika nusu fainali ya pili inayotarajiwa kupigwa saa 2:00 usiku leo, baada ya mchezo mwengine wa hatua hiyo utakaotangulia wakati wa saa 12:00 jioni ambao utazikutanisha timu za Provence na wenyeji Kurdistan.
Zanzibar Heroes imeshika usukani wa kundi B, ikiwa na pointi sita na magoli tisa, ambapo awali iliichapa Raetia mabao 6-0.
Cyprus ya Kaskazini imeingia nusu fainali licha ya juzi kufungwa mabao 2-1 na Provence, ikishika nafasi ya pili ya kundi hilo ikiwa na idadi kubwa ya magoli baada ya kuishindilia Darfur magoli 15-0 katika mchezo wa kwanza wa kundi C.
Darfur imeshatolewa kufuatia kupokea kipigo chengine cha mabao 18-0 mbele ya Provence.
Michezo yote ya nusu fainali inatarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Duhok.
Kila la kheri!
ReplyDelete