Habari za Punde

Makundi Copa Coca Cola hadharani


 Dar es Salaam
MAKUNDI ya timu zitakazoshiriki michuano ya soka kwa vijana Copa Coca Cola, yametangazwa jana, huku timu ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba, zikiwa katika kundi B.

Sambamba na hizo, timu nyengine zinazounda kundi hilo ni Iringa, Manyara, Morogoro, Mwanza na mkoa wa Tanga.

Kundi A lina timu za Arusha, Ilala, Kigoma, Kusini Pemba, Lindi, Rukwa na Ruvuma, ambappo kundi C linajumuisha timu za mikoa ya Dodoma, Kaskazini Unguja, Kinondoni, Mara, Mbeya, Mtwara na Temeke, wakati kundi D ni Kagera, Kilimanjaro, Kusini Unguja, Pwani, Shinyanga, Singida na Tabora.

Michuano hiyo ngazi ya Taifa inaanza kutimua vumbi Juni 24 mwaka huu kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa pambano la kukata utepe kuzikutanisha timu za Kigoma na Lindi kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Upangaji ratiba ya patashika hizo ulifanyika jana kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kushuhudiwa na waandishi wa habari, makocha wa timu za mikoa za Copa Coca-Cola na wadhamini kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola.

Makocha 35 wa timu za Copa Coca-Cola kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani wako kwenye kozi ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), inayoendeshwa na wakufunzi Ulric Mathiot wa FIFA kutoka Seychelles na wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Sunday Kayuni wa Tanzania.







No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.