Na Issa Mwadangala.
Wafanyabiashara na wafugaji katika Kijiji cha Kasinde Kata ya Kapele Wilaya ya Momba Mkoani Songwe wametakiwa kuacha mara moja tabia ya kununua au kuuza mifugo ya wizi, kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai linaloweza kuwasababishia adhabu kali ya kisheria.
Elimu hiyo imetolewa Julai 13, 2025 na Polisi kata wa kata hiyo Mkaguzi wa Polisi Stephen Tarimo wakati akitoa elimu kwa wafanyabiashara na wafugaji hao katika Mnada wa Kasinde kuhusu athari za ununuaji wa mali za wizi, hususa ni mifugo.
“Na toa rai kwenu msinunue mifugo bila kuwa na vielelezo halali kama stakabadhi ya mauzo na barua kutoka kwa uongozi wa kijiji, ni kosa kununua mifugo bila kufuata utaratibu wa kisheria na ukikamatwa utachukuliwa kama mshirika wa wizi,” alisema Mkaguzi Tarimo.
Aidha, Mkaguzi Tarimo alitoa wito kwa wafugaji kuhakikisha wanachukua hatua stahiki za kiusalama ikiwa ni pamoja na kuweka alama za utambuzi kwa mifugo yao ikiwa ni pamoja na kushirikiana na viongozi wa vijiji kuripoti matukio ya wizi wa mifugo mapema, na kujiepusha na tamaa ya kuuza mifugo kwa watu wasiofahamika kwani wapo watu wanatumia njia hiyo kutakatisha fedha halamu ili ziwe halali.
Kwa upande wao, baadhi ya wafungaji na wafanyabiashara hao waliohudhuria kwenye mnada huo walieleza kufurahishwa na elimu hiyo, wakiahidi kushirikiana na Jeshi la Polisi kukomesha wizi wa mifugo unaoathiri maisha ya wafugaji na uchumi wa jamii kwa ujumla.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea kutoa elimu katika makundi mbalimbali katika jamii ili kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa wa kutosha na kuchukua hatua za kulinda mali zao pamoja na kusaidia kukomesha wizi wa mifugo.
No comments:
Post a Comment